January 10, 2013

TAFF YAWASHUKURU WATANZANIA, YAKANUSHA KIFO CHA VENGU


Na Elizabeth John
SHIRIKISHO la Filamu Tanzania (TAFF), limetoa shukrani kwa Watanzania kwa ushiriki wao katika hatua zote za maradhi, msiba na mazishi ya aliyekuwa msanii mwenzao, Said Juma Kilowoko ‘Sajuki’.

Sajuki alianza kusumbuliwa na tumbo Septemba 2011 ambapo TAFF kwa kushirikiana na wadau wa filamu nchini, pamoja na viongozi mbalimbali wa serikali walimsaidia kumpeleka India kwaajili ya matibabu.

Akizungumza jijini Dar es Salaam, Rais wa TAFF, Simon Mwakifwamba alisema baada ya kutoka India alipata nafuu na Desemba mwaka jana akauugua ghafla ugonjwa wa kansa ya ngozi hadi alipofikwa na umauti Januari 2 mwaka huu.

“Kifo cha Sajuki kiliwavuta Watanzania wengi hasa kutokana na historia ya maradhi kwa muda mrefu, TAFF tunawashukuru wote ambao waliweza kushiriki kwa hali na mali kipindi chote cha maradhi mpaka umauti, hatuwezi kumkumbiuka kila mmoja kwa nafasi yake,” alisema Mwakifwamba.

Mwakifwamba alisema arobaini ya Sajuki itafanyika Februali 8 mwaka huu nyumbani kwake Tabata jijini Dar es Salaam.

Aidha, TAFF wamewataka Watanzania kuendelea kushirikiana na wasanii katika nyanja tofauti, ikiwa ni pamoja na vyombo vya habari kuendelea kutoa habari zinazohusu tasnia ya filamu ambazo zitaonya, kuelimisha na kukumbusha wajibu wa wasanii katika jamii kwa maendeleo ya taifa letu.

Katika hatua nyingine, Mwakifwamba alikanusha taarifa ya kifo cha msanii wa kundi la Komedi Joseph Shamba ‘Vengu’ zilizosambaa kwa watu mbalimbali pamoja na baadhi ya vyombo vya habari.

“Mwenyewe taarifa hizo nimezipata, lakini sio kweli, tumuombee apone haraka kwani hali yake bado mbaya anasumbuliwa na mtikisiko wa ubongo, kuna muda anapoteza fahamu,” alisema Mwakifwamba. 

No comments:

Post a Comment

Pages