January 09, 2013

ZAMBIA YATANGAZA WATAKAOTETEA UBINGWA WA AFCON


LUSAKA, Zambia

Zambia itaanza harakati za kuutetea ubingwa wao dhidi ya Ethiopia hapo Januari 21, kabla ya kuivaa Nigeria Januari 25 na kumaliza mechi za makundi dhidi ya Burkina Faso hapo Januari 29 kwenye Uwanja wa Mbombela, mjini Nelspruit

KOCHA wa mabingwa wa soka barani Afrika, timu ya taifa ya Zambia ‘Chipolopolo,’ Herve Renard ametangaza majina ya nyota 23 wa nchi hiyo watakaotetea ubingwa Mataifa Afrika nchini Afrika Kusini waliotwaa Februari 2012, jijini Libreville, Gabon.

Renard amewaacha kikosini beki mkongwe Chintu Kampamba, Salulani Phiri na Shadreck Malambo, katika orodha yake aliyokabidhi kwa Shirikisho la Soka Afrika (Caf) juzi Jumanne.

Saa chache kabla ya kutangaza kikosi chake, Renard alimuita kikosini mlinda mlango Danny Munyau kujaza nafasi ya Kalililo Kakonje, ambaye aliumia Jumapili kwenye mazoezi ya timu hiyo na kuondoshwa.

Renard anaugulia vichapo vitatu ilivyoambulia timu yake, katika mechi za majaribio dhidi ya timu za taifa za Tanzania, Angola na Morocco, alizozitumia kupata wakali wa kikosi chake.

Keshokutwa Januari 12, Renard mshindi wa tuzo ya Kocha Bora wa Mwaka barani Afrika, ataiongoza Chipolopolo kucheza pambano la kirafiki dhidi ya timu ya taifa ya Norway, litakalopigwa kwenye dimba la Levy Mwanawasa jijini Ndola.

Zambia itaanza harakati za kuutetea ubingwa wao dhidi ya Ethiopia hapo Januari 21, kabla ya kuivaa Nigeria Januari 25 na kumaliza mechi za makundi dhidi ya Burkina Faso hapo Januari 29 kwenye Uwanja wa Mbombela, mjini Nelspruit.

Kikosi cha Renard kinaundwa na walinda mlango; Kennedy Mweene, Joshua Titima na Daniel Munyau, wakati mabeki ni Stopilla Sunzu, Hichani Himonde, Francis Kasonde, Davies Nkausu, Joseph Musonda na Emmanuel Mbola.

Viungo ni: Rainford Kalaba, Nathan Sinkala, Mukuka Mulenga, Isaac Chansa, Chisamba Lungu, Felix Katongo, Noah Chivuta na William, Njobvu, huku washambuliaji wakiwa ni Emmanuel Mayuka, Collins Mbesuma, Jacob Mulenga, James Chamanga, Jonas Sakuwaha na nahodha Christopher Katongo.

No comments:

Post a Comment

Pages