March 27, 2013

EAST AFRICA BAR MABINGWA MASHINDANO YA NYAMA CHOMA MOSHI

 Mashabiki wa Bar ya East Africa wakishangilia mara baada ya kutangazwa washindi wakati wa shindano la Safari Nyama Choma lililofanyika katika Viwanja vya CCM Mkoa Mwishoni mwa wiki.
Mkuu wa Wilaya ya Moshi, Dr.Ibrahim Msengi (wa pili kulia) akimkabidhi kitita cha sh. milioni moja Meneja wa Bar ya East Africa,Godfrey Mawala (kulia), baada yakuibuka washindi wa kwanza katika shindano la Safari Lager Nyama Choma lililofanyika Moshi Kushoto ni Meneja wa Bia ya Safari Lager, Oscar Shelukindo.Wapili kulia ni Mpishi Mkuu Wilfred William na Meneja Mauzo wa Moshi, Edmundi Rutaraka

Na Mwandishi Wetu, Moshi

EAST AFRICA BAR, wametwaa ubingwa wa mashindano ya Nyama Choma Mkoa wa Moshi, baada ya kuzigaragaza baa nne zilizotinga fainali ya mashindano hayo yanayodhaminiwa na Kampuni ya Bia Tanzania (TBL) kupitia bia ya Safari Lager.

Kwa kutwaa ubingwa huo katika fainali zilizofanyika juzi Jumapili kwenye Viwanja vya CCM Mkoa , baa hiyo ilizawadiwa fedha taslim Sh milioni moja pamoja na cheti.

Waliokuwa mabingwa watetezi wa mashindano hayo mkoani hapa, Makanyaga Bar, walishika nafasi ya pili na kuondoka na kitita cha Sh 800,000 na cheti, wakati White Star Pub walishika nafasi ya tatu na kupata zawadi ya Sh 600,000 na cheti.

Walioibuka na nafasi ya nne ni baa ya Forest Bar iliyozawadiwa Sh 400,000 na cheti, wakati baa ya Lamina ilishika nafasi ya tano na kuzawadiwa Sh 200,000 na cheti.

Akizungumza kabla ya kumtangaza mshindi, Jaji Mkuu wa fainali hizo, Douglas Sakibu, alisema kuwa walitoa mafunzo kwa baa zote hizo juu ya mambo wanayopaswa kuzingatia katika uchomaji nyama.

Alivitaja vigezo walivyotumia kupata mshindi kuwa ni usafi wa mchomaji, vifaa na mazingira, maandalizi ya nyama kuanzia uchaguzi, uhifadhi wake na wa vifaa.

Vingine ni uchomaji na upangaji nyama, ladha na ulaini wake, mazingira ya eneo, mtiririko wa maji na uhifadhi wa taka.

Akizungumza kabla ya kumkaribisha mgeni rasmi, Meneja wa Bia ya Safari Lager, Oscar Shelukindo, alisema kuwa ni fahari kubwa kwa TBL na bia ya Safari Lager kwa ujumla kufanikisha shindano hilo mkoani ambao ndio mkoa wa mwisho.

“Tulianza kwa kuwataka watu wapige kura kupendekeza baa zinazofaa kuingia katika shindano la nyama choma kwa mkoa huu wa Moshi tukapata baa hizi tano zilizoingia fainali ambapo leo tutampata mshindi.

“Tunajua watu huwa wanakwenda katika baa na kula nyama hivyo tukaona ni vema tuanzishe mashindano haya ili walaji nyama choma wapate nyama bora,” alisema.

Alisema kuwa bia ya Safari Lager ina miaka takriani 36 na bado imeendelea kuwapo hadi sasa ambapo  ndio inayoongoza kwa mauzo.

Kwa upande wake, mgeni rasmi ambaye ni Mkuu wa Wilaya ya Moshi, Dr.Ibrahim    Msengi, aliisifu TBL kupitia Safari Lager kwa kuandaa mashindano hayo, akisema kuwa serikali inatambua mchango wa kampuni hiyo katika kujenga uchumi wa Taifa kupitia tukio hilo na mengineyo kama mashindano ya Pool Safari Lager, Safari Wezesha na hata udhamini wao katika michezo mbalimbali kama soka na mingineyo.

“Mashindano haya ni mazuri kwani yanawajengea wateja wa nyama mazingira mazuri na salama katika kutoa huduma hii ya nyama choma,” alisema.

Alizitaka baa ambazo hazikufika fainali, kutokata tamaa na badala yake kujipanga kwa ajili ya mashindano ya mwakani, kwa kurekebisha yale waliyokosea mwaka huu.

No comments:

Post a Comment

Pages