March 20, 2013

Wanafunzi Sekondari Majani ya Chai hawajui kusoma

DAR ES SALAAM, Tanzania

SHULE ya Sekondari Majani ya Chai iliyoko wilayani Ilala, Dar es Salaam inakabiliwa na tatizo la baadhi ya wanafunzi wanaojiunga kutokujua kusoma kwa ufasaha.

Kauli hiyo ilitolewa jijini Dar es Salaam leo na Mwalimu Mkuu wa shule hiyo, Jasinta Assey, alipozungumza na waandishi wa habari kuhusu malalamiko yaliyotolewa na wazazi kuwa baadhi ya walimu wa shule hiyo hawafundishi ipasavyo, kitendo ambacho si kweli.

Alisema mfano mzuri ni matokeo ya mtihani wa kidato cha nne wa mwaka jana ambapo wanafunzi 76 kati 276 walikuwa hawajui kusoma, kitendo kilichoongeza idadi ya wanafunzi waliofeli katika shule hiyo.

“Walimu wa sekondari tuna kazi kubwa, kwani tunawapokea watoto ambao wengi wao wana matatizo ya kutojua kusoma na matokeo yake ni kushindwa kabisa kuzingatia masomo wawapo shuleni,” alisema.

Assey alisema  licha ya hilo, shule hivi sasa inakabiliwa na tatizo la baadhi ya wanafunzi wa kike na kiume kujiingiza kwenye vitendo vya utumiaji wa mihadarati hususan bangi ambayo imekuwa ikiuzwa na baadhi wakazi wanaoizunguka shule hiyo.

Alisema mfano mzuri ni juzi Jumanne,  wanafunzi  49 kati ya 54 wa kidato cha nne wanaosoma masomo ya sanaa walipotoroka darasani na kukutwa kwenye makundi ya wavuta bangi na kwamba  hivi karibuni mkazi mmoja aliokota nguo za mmoja wa wanafunzi alizokuwa amenyang’anywa na kutupwa vichakani.

Awali, baadhi ya wazazi walilalamika kuwa kuna walimu walioandaa muhtasari wa masomo yote kisha kuwauzia wanafunzi hao kwa gharama ya sh 1,000, ambapo pia imebainika kuwa ina makosa, hivyo kuwakaririsha watoto hao makosa.

No comments:

Post a Comment

Pages