September 26, 2013

AIRTEL YAPIGA JEKI MBIO ZA ROCK CITY MARATHON 2013
 Meneja Matukio wa Capital Plus, Mathew Kasonta (kulia) akifafanua jambo wakati wa mkutano na waandishi wa habari jijini Dar es Salaam leo. Katikati ni Meneja Uhusiano wa Airtel Tanzania, Bw. Jackson Mmbando na Ofisa Uhusiano CP, Geofrey Nangai.

Meneja Uhusiano wa Airtel Tanzania, Bw. Jackson Mmbando akionesha fomu za kujisajili kushiriki mbio hizo.  Kulia ni Meneja Matukio wa Capital Plus, Mathew Kasonta na Ofisa Uhusiano CP, Geofrey Nangai.

Na Mwandishi Wetu


KAMPUNI ya Simu za Mkononi ya Airtel ya Tanzania kupitia huduma ya Airtel Money, imetangaza kudhamini kwa mara ya tano mbio za Rock City Marathon zilizopangwa kufanyika Oktoba 27, jijini Mwanza, zikiwa na lengo la kukuza mchezo wa riadha nchini.

Airtel ni Mdhamini Mkuu wa mbio hizo kwa upande wa Mawasiliano, wakishirikiana na wadhaminiwa wengine NSSF, Africa Barrick Gold (ABG), Precision Air, Bank M, PPF, Nyanza Bottling Ltd, New Mwanza Hotel, Sahara Communications na Umoja Switch.

Akizungumza wakati wa hafla ya kutangaza udhamini huo iliyofanyika Makao Makuu ya Airtel jijini Dar es Salaam jana, Meneja Uhusiano wa Airtel Tanzania, Jackson Mmbando alisema kampuni yake imejipanga kusaidia shughuli mbali mbali za maendeleo ya jamii.

Kupitia udhamini huo, Mmbando aliongeza kuwa washiriki watajisajili moja kwa moja kupitia huduma ya Airtel Money na kutuma malipo yao ya fomu kwa kuandika neno MARATHON, kisha kuhifadhi ujumbe kama risiti kwa ajili ya kuonesha wakati wa kuchukua fomu katika vituo mbalimbali.

Mratibu wa Rock City Marathon 2013 zinazoratibiwa na Kampuni ya Capital Plus International, Mathew Kasonta, alisema kuwa mbio za mwaka huu zitakuwa kubwa na bora zaidi kwa kuleta pamoja washiriki kutoka ndani ya nje ya nchi.

“Tumeungana na Airtel, kupitia Airtel Money ili kutanua wigo wa ushiriki. Miaka iliyopita, watu wengi walikosa nafasi au kulazimika kusafiri umbali mrefu kwenda kwenye vituo tulivyoviandaa kununua fomu za usajili, kwa kupitia Airtel Money zoezi hili litakuwa limerahisishwa,” alisema Kasonta.

Alifafanua kuwa, baada ya mshiriki kutuma malipo kwa MARATHON (menu itakayopatikana katika Airtel Money), mtumaji atapokea ujumbe utakaomuonyesha pale utakapokwenda kuchukua fomu za usajili katika ofisi za Airtel jijini Dar es Salaam, Dodoma, Zanzibar, Mbeya, Arusha na Mwanza.”

Alisema kuwa washiriki wenye vigezo pia wataweza kusajili kwa kupata fomu zipatikanazo katika uwanja wa Nyamagana mkoani Mwanza, na katika ofisi za kampuni ya Capital Plus International zilizopo ghorofa ya tatu, upande wa kulia katika jengo la ATC, Mtaa wa Ohio jijini Dar es Salaam.


Kasonta alibainisha kuwa fomu za usajili zitapatikana katika viwango vya bei vifuatavyo; sh. 5,000 kwa mbio za km 21 (kwa watu wote) na sh. 3,000 kwa mbio za km 5 (kwa makampuni na taasisi), huku za km 3 (kwa wazee na watu wenye ulemavu wa ngozi) na mbio za km 2 kwa watoto (miaka 7 hadi 10) zitapatikana bure.

No comments:

Post a Comment

Pages