September 22, 2013

WALIOKUFA TUKIO LA UGAIDI KENYA WAFIKIA 59

Mmoja wa watu waliojeruhiwa katika shambulio la kigaidi nchini Kenya.

NAIROBI, Kenya

IDADI ya watu waliouawa katika shambulizi la kigaidi nchini Kenya, lililofanywa na wanamgambo wa kundi la Al-Shabaab imefikia 59 huku majeruhi nao wakiwa ni 175.

Waziri wa Usalama, Ole Lenku alisema kuwa idadi ya magaidi walio ndani ya jengo la Westgate ni kati ya 10 hadi 15 na kwamba bado haijulikani kama kuna watu wanazuiliwa.

Shirika la Red Cross awali katika taarifa yake lilisema kuwa watu 43 ndio waliofariki na zaidi ya 50 kujeruhiwa huku wengine wakitekwa nyara katika shambulizi hili la kigaidi lililotokea Jumamosi mchana.

Milio ya risasi ilisikika katika jengo la Westgate mjini Nairobi, ambako wanamgambo wa Al-Shabaab wanawazuilia mateka ambao idadi yao haijajulikana hadi sasa.

Wanajeshi wawili walijeruhiwa katika ufyatulianaji risasi na kukimbizwa hospitalini kwa matibabu, huku watu wawili wakinusuriwa leo asubuhi.

Hadi sasa jeshi limeweza kudhibiti hali nje na ndani ya jengo hilo, magari ya kijeshi yakiwa yamepelekwa katika eneo hilo huku polisi na wanajeshi wakijaribu kuwanusuru baadhi ya watu ambao bado wanazuiliwa ndani.

Watu 39 waliuawa baada ya wanamgambo hao kushambulia jengo hilo katika eneo la kuegeshea magari na kisha kuingia ndani ya migahawa na maduka katika jengo hilo lenye ghorofa nne na kuwapiga watu risasi kiholela.

Kuna taarifa kuwa wanamgambo hao wako ndani ya duka moja kubwa katika jengo hilo.

Rais wa Kenya, Uhuru Kenyatta amesema kuwa baadhi ya waliofariki ni jamaa zake.

Miongoni mwa waliofariki pia ni mwanadiplomasia wa Canada na raia wawili wa Ufaransa.

Rais Kenyatta alisisitiza kuwa wale waliohusika lazima wakabiliwe na mkono wa sheria.

Jamaa na marafiki waliofika kujua hali ya jamaa zao wamezuiwa kuingia ndani ya jengo hilo. Wengi wa waathiriwa walifariki kutokana na majeraha yao.

No comments:

Post a Comment

Pages