IDADI ya watu waliouawa katika shambulizi la kigaidi
nchini Kenya, lililofanywa na wanamgambo wa kundi la Al-Shabaab imefikia 59
huku majeruhi nao wakiwa ni 175.
Waziri wa Usalama, Ole Lenku alisema kuwa idadi ya magaidi
walio ndani ya jengo la Westgate ni kati ya 10 hadi 15 na kwamba bado
haijulikani kama kuna watu wanazuiliwa.
Shirika la Red Cross awali katika taarifa yake lilisema
kuwa watu 43 ndio waliofariki na zaidi ya 50 kujeruhiwa huku wengine wakitekwa nyara
katika shambulizi hili la kigaidi lililotokea Jumamosi mchana.
Milio ya risasi ilisikika katika jengo la Westgate mjini
Nairobi, ambako wanamgambo wa Al-Shabaab wanawazuilia mateka ambao idadi yao
haijajulikana hadi sasa.
Wanajeshi wawili walijeruhiwa katika
ufyatulianaji risasi na kukimbizwa hospitalini kwa matibabu, huku watu wawili
wakinusuriwa leo asubuhi.
Hadi sasa jeshi limeweza kudhibiti
hali nje na ndani ya jengo hilo, magari ya kijeshi yakiwa yamepelekwa katika
eneo hilo huku polisi na wanajeshi wakijaribu kuwanusuru baadhi ya watu ambao
bado wanazuiliwa ndani.
Watu 39 waliuawa baada ya
wanamgambo hao kushambulia jengo hilo katika eneo la kuegeshea magari na kisha
kuingia ndani ya migahawa na maduka katika jengo hilo lenye ghorofa nne na
kuwapiga watu risasi kiholela.
Kuna taarifa kuwa wanamgambo hao
wako ndani ya duka moja kubwa katika jengo hilo.
Rais wa Kenya, Uhuru Kenyatta
amesema kuwa baadhi ya waliofariki ni jamaa zake.
Miongoni mwa waliofariki pia ni
mwanadiplomasia wa Canada na raia wawili wa Ufaransa.
Rais Kenyatta alisisitiza kuwa
wale waliohusika lazima wakabiliwe na mkono wa sheria.
Jamaa na marafiki waliofika kujua
hali ya jamaa zao wamezuiwa kuingia ndani ya jengo hilo. Wengi wa waathiriwa
walifariki kutokana na majeraha yao.
No comments:
Post a Comment