September 25, 2013

Serikali na CCM zimekumbuka Shuka la Mauaji ya Nyamongo Asubuhi?

Na Bryceson Mathias
 
Naibu Waziri wa Nishati na Madini, Stephen Masele, na Katibu Mkuu wa Chama cha Mapinduzi (CCM), Abdulahmana Kinana, ni kama wamekumbuka shuka asubuhi kuhusu mauaji ya wananchi wa Nyamongo dhidi ya Wawekezaji wa Mgodi wa dhahabu wilayani Tarime.
Akifafanua mambo kadhaa wakati wa ziara ya CCM iliyofanywa na Kinana ambayo Masele alidai Wizara yake itataka wananchi wafaidike na migodi ikiwa ni pamoja na kuwasaidia wachimbaji wadogowadogo, ambapo amesema wanatakiwa wajiunge katika vikundi.
Mbali ya wananchi wa Nyamongo kumshukuru Katibu Mkuu wa CCM, Kinana, na Katibu wa NEC Itikadi na Uenezi wa CCM, Moses Nnauye, waliodiriki kuweka rehani nyadhifa zao iwapo kero za wananchi hao hazitatatuliwa, naona ni kama Serikali ya CCM imekumbuka Shuka la Mauaji ya Nyamongo Asubuhi.
 
Rai yangu, Kinachotakiwa sasa si kuruka viunzi, kutoa ulaghai na kukataa ‘Hata mimi sifurahishwa na mauaji na ujenzi wa Ukuta wa Gharama uliojengwa na wawekezaji’ kama alivyokuwa akijiosha Masele, kinachotakiwa ni kukomesha mauaji, Vitisho na Kero dhidi ya wakazi wa Nyamongo.
 
Ingawa Kinana alitumia Demokrasia ya hali ya juu kuwapa nafasi watu watatu ambao wananchi waliwachagua waelezee Kero na matatizo yanayowakabili akiwepo mkazi wa Nyamongo, Chacha Magayo Butora, dhidi ya mwekezaji, bado haifuti simanzi, kilio na machungu ya mauaji yaliyowatokea.
 
Waswahili wanasema, Ukiona Nyani Kazeeka! Amekwepa Mishale Mingi! Kama wananchi wa Nyamongo wanaweza wakawapanga watu kuongelea Kero zao kwa ufasaha kwa majina ili kuwasemea, ujue wanafahamu wanachokidai, ambako ni kukomeshwa kwa mauaji na umwagaji damu.
 
Mbali ya Mauaji, Kunyimwa Haki ya Uchimbaji Mdogo, wananchi hao wamepaza kilio Kingine ambacho Serikali na CCM havipaswi kutafuna maneno ila kushughulikia tatizo hilo, ni Wawekezaji kujenga Ukuta unaowatenganisha kwa gharama kubwa ambapo wanadai ingesaidia maendeleo.
 
Kutokana na wananchi wa Nyamongo kupatwa na madhara mengi, Mauaji na adha nyingi dhidi ya mwekezaji wa Mgodi huo ambayo si mageni masikioni na machoni mwa watanzania, kimsingi si wakati muafaka kwa wanasiasa kuanza kuwalaghai na matamko yasiyo na mashiko.
 
Mwana mpotevu baada ya kujitambua, alirudi kwa Baba yake akasema nimekosa mbele yako na mbele ya Mungu na akasema sistahili kuitwa mwana wako, ila unifanye kuwa mmojawapo wa watumwa wako ili aendelee kula, kuvaa na kulala nyumbani kwa Babaye.
 
Ni saa ya Serikali na CCM kurudi kwa Waajiri wao wananchi wa Nyamongo na kuwaomba radhi kwa yaliyotokea ndani ya Utawala wake, ili wananchi hao wawapokee na wawavike mavazi mazuri na pete, ingawa rasilimali na tija ya wana nyamongo, imetapanywa kwa Wawekezaji hao na wakati mwingine imetumika vibaya kuwaumiza!.
 
Si muda muafaka kumtafuta Waziri wa Mambo ya Ndani, Emmanuel Nchimbi, tena na  kukumbusha machungu yaliyopita yatakayozua mabishano yasiyo na tija.
 

No comments:

Post a Comment

Pages