February 04, 2014

Ali Kiba: ‘Collabo’ na Diamond haitatokea

Na Elizabeth John
NYOTA wa muziki wa kizazi kipya nchini, Ali Kiba amesema kufanya ‘Collabo’ na msanii wa muziki huo, Naseeb Abdul ‘Diamond Platinum’ haitakuja kutokea katika maisha yake.

Kauli hiyo ya Ali Kiba imekuja baada ya mashabiki wa muziki huo, kumshauri afanye kazi na msaniii huyo kwa kushirikiana na msanii mwenzao Omary Nyembo ‘Ommy Dimpoz’ na kuibashiri kwamba itakua kazi nzuri kutokana na vipaji walivyonavyo wakali hao.

Akizungumza jijini Dar es Salaam jana, Ali Kiba alisema amekuwa akipokea maoni mbalimbali kutoka kwa mashabiki wake lakini hicho kitu hakiwezi kutokea kamwe.

“Kiukweli sifikirii na sidhani kama itakuja kutokea kwani kufanya kazi na Diamond ni mfano wa kudeki bahari haitakuja kutokea kamwe, naomba wapenzi wangu waangalie kazi nyingine nitakazotoa sio kusubiri kufanya kazi na msanii huyo ni kama ndoto,” alisema.

Ali Kiba ni kati ya wasanii ambao wanafanya vizuri katika tasnia ya muziki huo kutokana na kipaji chake cha kutunga mashairi ambayo yanavutia na kuliteka soko la muziki huo.

Msanii huyo kwasasa anatamba na kibao chake kinachojulikana kwa jina la ‘Kujiinamia’ ambacho ameshirikiana na mdogo wake, Abdu Kiba.

No comments:

Post a Comment

Pages