February 14, 2014

Hatutasimamisha mgombea dhaifu Kalenga na lazima CCM ianze kuzoea kushindwa-Chadema

 Mkurugenzi wa Operesheni na Mafunzo wa Chadema, Benson Kigaila akizungumza na  wajumbe wa  mkutano wa Halmashauri kuu ya  Chadema jimbo la Kalenga jana huku  akionyesha katiba ya  Chadema   kabla ya  wajumbe  wa mkutano huo  kupiga  kura  kumchagua mgombea ubunge  jimbo hilo kupitia Chadema. (Picha na Francis Godwin)  
Wajumbe  wa mkutano wa kura za maoni Chadema  jimbo la Kalenga  wakiwa katika ukumbi wa St Dominic. 


Francis Godwin na Denis Mlowe  Iringa 

WAKATI jana  wajumbe  wa  Halmashauri kuu ya  chama cha  Demokrsia na maendeleo (CHADEMA)   jimbo la  Kalenga  wameshiriki katika zoezi la  upigaji wa  kura za maoni kuchagua mmoja kati ya  wanachama 13 waliojitokeza  kurejesha  fomu  za  kuomba  kuteuliwa kuwa wagombea wa nafasi ya  ubunge  jimbo la kalenga kupitia  chama hicho ,mkurugenzi wa Operesheni na Mafunzo wa Chadema, Benson Kigaila amesema chama  chake kamwe hakitasimamisha mgombea dhaifu  katika kinyang'anyiro hicho na lazima  CCM kianze kuzoea kushindwa .

Huku  mbunge  wa viti  maalum mkoa wa Iringa na mjumbe wa kamati kuu  ya  Chadema Bi Chiku Abwao akiwataka  wana Kalenga  kujenga  imani  na Chadema na kuwa haitakuwa  tayari  kumweka  ndugu  katika chaguzi  hizo na  kuwa CCM imeonyesha  kuwadharau  wana Kalenga  kwa kuendekeza  siasa za familia katika  jimbo  hilo jambo ambalo halikubaliki.

Akifungua  mkutano huo wa  kura za maoni  katika ukumbi wa St Dominic mjini Iringa Kigaila alisema  kuwa  lengo la mkutano huo  ni kuanzisha mchakato  wa  kumpata  mgombea  wa Chadema na kuwa Chadema ina matumaini makubwa ya  kushinda katika  jimbo hilo.

" CCM    walikuwa  wakisikilizia ni  nani  ambae Chadema itamsimamisha katika  jimbo hilo na  kuwa  walidhani  wapo peke yao  ila  sasa Chadema inatangaza  rasmi  kuwa  mchakato wa  kumpata  mgombea  wake  umeanza  na ni lazima apatikane mgombea ambae  atakuwa ni  tofauti  na mgombea wa CCM....lazima CCM kwa  hapa  kilipofika   kianze  kuzoea kushindwa katika  uchaguzi"

Alisema  kuwa  utaratibu  wa kumpata mgombea wa  Chadema ni utaratibu ambao hautokani na mtu  mmoja ama  viongozi  pekee  wa  juu bali ni utaratibu  shirikishi ambao baada ya  kutoka katika hatua ya  kura za maoni  kitafuata  kikao  cha kamati ya  utendaji ya jimbo kabla ya kamati kuu ya  chama kufanya maamuzi  yake Februari 14 jijini Dar es Salaam kwa kumteua  mgombea atakayesimama jimbo hilo la Kalenga.

Hivyo  aliwataka   wana Chadema  kuwa makini katika  kusikiliza  kila mgombea na kuhakikisha  wanachagua  mgombea ambae atakubalika katika chama  hicho na hata  vyama vingine  kikiwemo CCM na  wananchi  wote wa   jimbo la Kalenga.

Kigaila  alisema mchakato  wa  kuchukua fomu ndani ya  chama  hicho jumla ya  wana Chadema 16  walijitokeza kuchukua fomu  ila hadi  juzi siku ya mwisho  kurejesha fomu ni  wanachama 13  ndio  ambao walirejesha  na  kudai  kuwa mwitikio  huo ni ishara nzuri ya  Chadema kuonyesha  kukua  zaidi  katika jimbo la Kalenga.

Hata  hivyo  alisema  kuwa  Chadema kina imani kubwa ya  kushinda  kiti  hicho  cha jimbo la Kalenga na  ushindi  huo  utakuwa ni mwanzo wa  kukiondoa  chama  tawala madarakani .

Kwa  upande wake  Abwao  alisema  kuwa  CCM kimewasaliti  wananchi  wa  jimbo la Kalenga  kwa   kuonyesha  kuibeba  familia ya aliyekuwa  mbunge wa  jimbo  hilo Dr  Wiliam Mgimwa na  kuwaomba  wana Kalenga  kuunganisha  nguvu  zao kumchagua mgombea wa Chadema atakayeteuliwa na Chama .

Awali  katibu  wa Chadema wilaya ya  Iringa vijijini Felix Nyondo aliwataja  waliojitokeza  kuchukua na kurejesha  fomu  kuwa ni pamoja na Zubery Mwachura , Dr Evaristo Mtitu, Akbar Sanga, Grace Tendega, Rehema Makoga, Sinkala Mwenda, Henry Kavina, Aidan Pungili, Mussa Mdede, Mchungaji Samweli  Nyakunga,  Daniel Luvanga, Anicent Sambala na Vitus Lawa.

Hata  hivyo   wagombea  12  ndio  waliofika  ukumbini  hapo  huku mgombea mmoja  Zubery Mwachura akikosekana   kutokana na  kuwa  nje  ya nchi kwa  shughuli  za kikazi.

1 comment:

Pages