February 16, 2014

Tunu za taifa ziongezwe-Vijana
BAADHI ya vijana nchini wamewataka wajumbe wa Bunge Maalumu la Katiba kupigania ili tunu za taifa ziongezwe katika Ibara ya kwanza kifungu cha tano.

Tunu ambazo wametaka ziongezwe ni ardhi na amani.
 Wakizungumza kwa nyakati tofauti jijini Dar es Salaam mwishoni mwa wiki, vijana hao walisema bila ya kuwa na utaratibu maalumu wa umiliki wa ardhi kuna hatari nchi kuingia kwenye machafuko.

Walisema wamefikia hatu hiyo baada ya kubaini vifungu  hivyo muhimu vimeachwa kwenye rasimu ya pili ya katiba itakayoanza kujadiliwa bungeni kesho.

Mmoja wa vijana hao, Amos Joseph, alisema ardhi na amani ni vitu muhimu kwa maisha ya Watanzania, hivyo kutofanywa tunu za taifa ni jambo la hatari.

 “Rasimu inatamka Jamhuri ya Muungano itaenzi na kuzingatia Tunu za Taifa ambazo ni utu, uzalendo, uajibikaji, umoja, uwazi uwadilifu na lugha ya taifa, huku ardhi na amani vikiachwa na ambavyo ni vitu muhimu katika mustakabali wa nchi yetu,”alisema Joseph.

Matrida Thobias, ambaye ni mlemavu wa kutosikia (kiziwi), mkazi wa Mabibo, alisema pamoja na kuwa Watazania bado wanaendelea kuienzi amani na kuilinda ,lakini anaamini umefika wakati wa amani kuingizwa kwenye kifungu hicho.

Alisema machafuko mengi wanayoyasikia yakitokea  kwenye baadhi ya nchi duniani yamekuwa yakichangiwa na amani kutofanywa kuwa Tunu ya Taifa.

No comments:

Post a Comment

Pages