October 20, 2014

Mke wa Makamu wa Pili wa Rais wa Zanzibar Mama Asha Iddi afungua Baraza Kuu la Umoja wa Wanawake Tanzania (UWT) Mjini Zanzibar.

 Mke wa Makamu wa Pili wa Rais wa Zanzibar Mama Asha Suleiman Iddi akifurahia kazi za amali zinazofanywa na  akina Mama wa Vikundi vya Ushirika vya Jimbo la Magomeni na kushawishika kununua mkeka wa asili ya Zanzibar.
 Baadhi ya Wajumbe wa Baraza Kuu la Umoja wa Wanawake Tanzania { UWT } Jimbo la Magomeni wakisikiliza hotuba ya Mgeni Rasmi Mke wa Makamu wa Pili wa Rais wa Zanzibar Mama Asha Suleiman Iddi hayupo pichani akilifungua Baraza hilo.
Mama Asha Suleiman Iddi akilifungua Baraza Kuu la UWT Jimbo la Magomeni kwe3nye Ukumbi wa Ofisi ya CCM Tawi la Nyerere Mjini Zanzibar. (Picha na Hassan Issa wa OMPR – ZNZ).

xxxxxxxxxxxxxxxxxxxxxxxxxxxxxxxxxxxxxxxxxxxxxxxxx

Akinamama nchini wana wajibu wa kujiepusha na makundi ambayo ndio adui mkubwa  katika harakati za maendeleo na Kisiasa hasa wakati huu wa Taifa likikaribia kuelekea katika uchaguzi Mkuu ujao wa mwaka 2015.

Mke wa Makamu wa Pili wa Rais wa Zanzibar Mama Asha Suleiman Iddi alisema hayo wakati akilifungua Baraza Kuu la Umoja wa Wanawake Tanzania  (UWT) Jimbo la Magomeni linalofanyika katika ukumbi wa Ofisi ya Tawi la CCM Nyerere Wilaya ya Mjini Zanzibar.

Mama Asha alisema njia pekee ya kufikia maendeleo hayo ni kwa akina mama hao pamoja na wananchi wote kufanya kazi zao kwa bidii na maarifa ili kufikia malengo wanayojipangia kuyatekeleza.

Alisema kamwe hakutakuwa na miujiza itakayoletwa na baadhi ya watu kwa kutaka kufanikisha maslahi yao binafsi kupitia udanganyifu wanauelekeza kwa  wananchi hasa wanawake ili kufikia azma yao.

Mama Asha alifahamisha kwamba CCM ndio chama pekee Nchini Tanzania chenye uwezo wa kuwaletea maendeleo wananchi kutokana na sera zake zenye uwezo wa kutekelezeka wakati wote.

Aliwatahadharisha akina mama hao kuwa na tahadhari  na watu waliowahi kuneemeka na Serikali zilizopo madarakani ambao wakati huu wamekuwa wakizipinga kwa vile wako nje ya utumishi.

Alieleza kwamba ushawishi wa watu hao ulifikia hatua ya kuwataka watu wawe vilema kwa sababu tu ya uchu wao wa madaraka ya nchi hii bila ya kujali kuwa vitendo vyao hivyo vina muekeo wa kujenga chuki za maisha ndani ya jamii.

Katika kuunga mkono vikundi vya kiuchumi na ushirika vya akina mama hao wa Jimbo la Magomeni Mama Asha alisema kupitia Umoja wao wa Wake wa Wawakilishi na Wabunge wa CCM Zanzibar wataangalia uwezekano wa kusaidia akina mama hao.

Aliuomba uongozi wa Umoja wa Wanawake Tanzania { UWT } Jimbo la Magomeni kuviorodhesha vikundi hivyo pamoja na muongozo wa shughuli wanazozifanya akina mama hao ili vipatiwe msaada unastahiki kutokana na kazi zao.

Mapema akitoa taarifa fupi ya Umoja wa Wanawake Tanzania Jimbo la Magomeni Katibu wa UWT Jimbo hilo Bibi Maimuna Bara bara alisema akina mama wa Jimbo hilo wako imara kuisubiri Katiba iliyopendekezwa na Bunge la Katiba kwa ajili ya kuipigia kura ya ndio wakati ukiwadia.

Bibi Maimuna alisema akina Mama hao wamewapongeza Wajumbe wa Bunge Maalum la Katiba kwa uwamuzi wao wa kupendekeza Katiba inayotoa fursa sawa ya hamsini kwa hamsini kijinsia kwenye nafasi za uongozi pamoja na maamuzi ya Taifa.
Alisema katika kukabiliana na ukali wa kimaisha akina mama wa Jimbo hilo tayari wameshaanzisha vikundi 11 vya kuweka na kukopa sambamba pia na kuanzisha vikundi vya vikoba.

Hata hivyo Bibi Maimuna alieleza kwamba zipo changa moto zilizojitokeza katika vikundi vyao akizitaja kuwa ni pamoja na ufinyu wa elimu kwa wana vikundi, vitendea kazi kama Kompyuta pamoja na ukosefu wa fedha za kuendeshea miradi yao.


Othman Khamis Ame
Ofisi ya Makamu wa Pili wa Rais wa Zanzibar
20/10/2014.

No comments:

Post a Comment

Pages