October 10, 2014

TAKUKURU YATAKA USHIRIKIANO KATIKA KUPAMBANA NA RUSHWA

TAASISI ya Kuzuia, Kupambana na Rushwa (Takukuru), imesema katika kumuenzi Mwalimu Nyerere dhidi ya rushwa, Watanzania wanatakiwa kutoa ushirikiano katika kuwataja baadhi ya watu wanaojihusisha na vitendo hivyo baadala ya kulalamika tu.

Mkuu wa Elimu ya Raia kwa Umma wa Takukuru, Stella Mpanju, aliyasema hayo juzi, wakati wa Kipindi cha Malumbano ya Hoja kinachorushwa na kituo cha luninga cha ITV, akibainisha kwamba mapambano dhidi ya rushwa ni ya Watanzania wote.

Alisema, itakuwa ni makosa kwa baadhi ya watu kufikiria kuwa Takukuru itafanikiwa katika mapambano hayo bila ya ushirikiano wa wananchi ambao anaamini wanawajua wala rushwa katika maeneo yao.

“Mnawajua wanaojihusisha na vitendo vya vya ulaji rushwa kwani miongoni mwenu mnawajua sasa bila kuwataja itakuwa ni vigumu kwa watu hao kuchukuliwa hatua, haiwezekani Takukuru ikajikamatia watu bila ya kuwa na ushahidi, haya ni masuala yakisheria, watajeni halafu mtuachi hiyo kazi sisi,”alisema Stella.

Aliongeza kwa wataka kuacha kulalamika na kuitupia lawama Takukuru huku wakisahau wajibu na uwajibikaji katika kuzuia vitendo hivyo,ambapo  baadhi yao ndio  chachu vitendo hususan wanapohitaji kupatiwa uhuduma kwenye maeneo mbalimbali yanayotoa huduma.

“Wote hapa mnalalamikia vitendo hivyo, lakini huwa najiuliza mla rushwa ni nani, hata nyie hapa nikiwauliza nani anakula rushwa wote hapa hamtakuwa na jibu, ni lazima tukaelewa kuwa vita hii inahitaji ushirikiano na jamii ibadili mitazamo dhidi ya mapambano haya.

Awali mmoja wa shiriki aliyejitaja kwa jina moja la Likwepa aliwataka Takukuru kuacha kukukwepa majikumu yao, kuwaachia wananchi kazi yao ambayo inawafanya wapate mishahara.

“Jamii inapokosa maadili inaogopa kupambana na watu wanaokula rushwa, pia rushwa imekuwa sana baada ya kuanzishwa Azimio la Zanzibar ambalo lilivunja mihimili yote ya Azimio la Arusha,”alisema Likwepa.


Gervas Lutaguzinda, mshiriki katika mjadala huo, alisemakosa kubwa walilofanya watawala wa sasa ni kuua Azimio la Arusha ambalo lilikuwa na miiko ya uongozi, iliyoongoza mapambano dhidi ya rushwa.

“Mfano mwl Nyerere aliwtaka viongozi wa serikali wasijihusishe na biashara, lakini baada ya kuvunjwa azimio la Arusha siasa za nchi hii zinaendeshwa na wafanyabiashara ambao wamekuwa wakitumia rushwa kununua ubunge, udiwani na vyeo. vingine,”alisema.

No comments:

Post a Comment

Pages