November 05, 2014

MKUU WA MKOA WA TANGA AWATAKA WANAWAKE KUWEKEZA KATIKA ARDHI

Ofisa Wakala wa Nje kutoka Mfuko wa Hifadhi ya Jamii  PPF, Pima Mohamed akitoa maelezo ya huduma zinazotolewa na mfuko huo kwa Mkuu wa Mkoa wa Tanga,  Chiku Gallawa (katikati) alipotembelea banda hilo wakati wa ufunguzi wa Kampeni  ya Mwanamke na Uchumi iliyofanyika jijini Tanga na kuandaliwa na  Kampuni ya Angels Moment. Kulia ni Mkurungenzi wa kampuni hiyo,  Naima Malima. (Picha na Elizabeth Kilindi)
 

NA ELIZABETH KILINDI, TANGA
 
WANAWAKE wajasiriamali  Mkoani  Tanga wametakiwa kuwekeza kwenye ardhi ili kuweza kujikwamua kiuchumi kwani  kilimo ni mkombozi  katika kuinua uchumi.


Rai hiyo imetolewa na Mkuu wa Mkoa wa Tanga Chiku Gallawa wakati wa semina ya kampeni ya mwanamke na uchumi  iliyoandaliwa na kampuni Angels Moment katika ukumbi wa Naivera ambapo alitolea mfano katiba ya sasa ambayo imetoa kipaumbele cha mwanamke kumiliki Ardhi.


Mkuu wa Mkoa huyo alisema wanawake wamekuwa wakijishughulisha na na shughuli mbalimbali  za mikono lakini zimekuwa haziwaletei maendeleo ya haraka.


‘Wajasiriamali  wa Tanga wanafanya shughuli nyingi za mikono lakini maendeleo hayatokei kwa haraka na hivyo nawaomba nunueni Ardhi ambayo ni kitu cha kudumu na kilimo hakimtupi mtu hata siku moja’ alisema Gallawa.


Hata hivyo aliongeza kuwa shughuli za ujasiriamali ziungwe Mkono na kuhakikisha zinafanyika katika mazingira rafiki yatakayomsaidia
mwanamke.


Nae Mkurugenzi wa Kampeni  ya wanawake na uchumi  Mahada Erick alisema wanawake wajariamali wanakabiliwa na changamoto nyingi ikiwemo ukosefu wa mitaji na  uwezo mdogo  kuzitambua fursa zilizopo katika maeneo yao.


Aidha alisema kuwa jamii pia imekuwa ikishindwa kuwaunga mkono katika uwekezaji wa rasilimali ardhi  hali ambayo inasababisha wakinamama wengi kuogopa kushiriki katika Shughuli za kilimo.

No comments:

Post a Comment

Pages