November 05, 2014

MUONGOZO WA USHIRIKIANO KATIKA KUGOMBEA SERIKALI ZA MITAA, VIJIJI NA VITONGOJI KWA VYAMA VYA NLD, CHADEMA, NCCR-Mageuzi NA CUF


Katibu Mkuu wa Chama cha Demokrasia na Maendeleo (Chadema)Dk. Wilbrod Slaa akifafanua jambo wakati viongozi wakuu wa vyama vya NLD, NCCR-Mageuzi, CUF na Chadema waliposaini muongozo wa ushirikiano katika kugombea serikali za mitaa, vijiji na vitongoji. Wa pili kushoto ni Mwenyekiti wa CUF, Prof. Ibrahimu Lipumba na Mwenyekiti wa NCCR-Mageuzi, James Mbati. (Picha na Francis Dande)
 Mwenyekiti wa NCCR-Mageuzi, James Mbatia (kulia), Mwenyekiti wa CUF, Prof. Ibrahim Lipumba na Katibu Mkuu wa Chadema, Dk. Wilbrod Slaa wakionyesha mwongozo waliosaini wa ushirikiano katika kugombea serikali za Mitaa, Vijiji na Vitongoji kupitia Ukawa.
Mwenyekiti wa NCCR-Mageuzi, James Mbatia, Mwenyekiti wa CUF, Prof. Ibrahim Lipumba na Katibu Mkuu wa Chadema, Dk. Wilbrod Slaa wakisaini mwongozo wa ushirikiano katika kugombea serikali za Mitaa, Vijiji na Vitongoji kupitia Ukawa
 
Na Abdulrahman Lugone

Itakumbukwa kuwa vyama waanzilishi wa UKAWA walitiliana saini na kuamua kuweka mgombea mmoja kila ngazi ya uchaguzi utakaofanyika nchini kuanzia na uchaguzi wa serikali za mitaa, vijiji na vitongoji hapo Desemba 14, 2014.


Katika tamko la pamoja ambalo lilisainiwa na viongozi wakuu wa vyama iliamuliwa kuwa utaratibu rasmi wa vigezo na mfumo mzima wa kuweza kuachiana nafasi zinazogombewa utatumwa kwa wanachama na viongozi wa vyama vyetu ili uweze kutumika katika kuwapata wagombea katika nafasi mbalimbali ambazo zinagombewa .

Ili kuweza kufanikisha azima hiyo inashauriwa vigezo vifuatavyo viweze kutumika.

VIGEZO:
1. Chama kuwa na mgombea anaekubalika zaidi
2. Chama kilichoshinda uchaguzi uliopita 
3. Idadi ya wanachama
4. Maridhiano/muafaka au kura ya maoni 
5. Suluhisho la mwisho la mvutano wa mgombea
Utaratibu;

1. Kila CHAMA kilicho kwenye ushirika kinapaswa kuandaa wagombea (mwenyekiti na wajumbe) wenye sifa na wanaokubalika katika jamii, isipokuwa ni marufuku kwa chama kushawishi mwanachama wa chama kilichopo kwenye ushirika wa UKAWA kuhamia kwenye chama kingine.

2. Vyama vya ushirikiano viweke ratiba ya uteuzi wa wagombea wa ukawa kwa pamoja kwa ngazi husika.

3. Vyama vya ushirikiano vitatumia utaratibu wa mashauriano muafaka katika kumpata mgombea wa mtaa/kijiji/kitongoji; kwa kuwashindanisha wagombea kutokana na sifa na kukubalika kwao.

4. Sehemu ambayo Serikali ya kijiji/kitongoji/mtaa inayomaliza muda wake inaongozwa na mojawapo ya chama cha ushirikiano inaweza kuwa kigezo cha kuachiwa kuendelea kutetea kiti hicho, ila mradi mgombea/chama awe bado anakubalika.

5. Vyama vya ushirikiano vikishindwa kupata maridhiano/muafaka basi wanachama, na wapenzi wa vyama vyote (washirika) ngazi ya Tawi wapige kura ya awali ya pamoja kuamua wagombea wa uenyekiti na ujumbe.

6. Ngazi ya wilaya ya vyama shirika itakuwa msimamizi wa zoezi tajwa hapo juu (5).

7. Iwapo mgombea ameshateuliwa au kushindwa katika kura za maoni za moja ya chama shirika mtu huyo hatoruhusiwa kupokelewa na chama kingine cha ushirikiano; hii ni kuepusha migongano na mifarakano itakayopelekea ushirikiano kugawanyika na kupoteza nguvu ya umoja.

8. Vyama na viongozi wa ushirikiano, pamoja na wafuasi wao ni lazima vishiriki kwa ukamilifu katika kumnadi mgombea aliepitishwa na ushirikiano huo.

9. Baada ya Uchaguzi kumalizika, Uongozi wa Kitaifa wa vyama vinavyounda ushirikiano, vitaandaa kanuni ya pamoja ambayo italinda nidhamu kwa viongozi wote wa Serikali waliochaguliwa kupitia vyama vya mashirikiano, pindi uongozi huo ukienda kinyume na taratibu za kanuni hizo, chama husika kichukue hatua za kinidhamu dhidi ya kiongozi huyo.

Muongozo huu umekubaliwa na kutiwa sahihi na Viongozi wakuu wa Vyama vya ushirikiano vya NLD, NCCR-Mageuzi, CUF na CHADEMA tarehe 4 Mwezi Novemba, 2014.

No comments:

Post a Comment

Pages