Mratibu wa Shirika la Wanawake katika Maendeleo
barani Afrika (WiLDAF), Judith Odunga akifafanua jambo wakati wa akitoa taarifa
kuhusu Siku 16 za kupinga Ukatili wa Kijinsia, inayotarajiwa kuanza Novemba 25
hadi Desemba 10 mwaka huu. Kushoto ni Bahati Mandogo kutoka Kampuni ya JBS na Ofisa wa Polisi Dawati la Kijinsia, Christina Onyango.
Na Mwandishi Wetu
ASILIMIA 92 ya
wanawake nchini wametaka mila na utamaduni
unaolazimisha mwanamke akeketwe ukomeshwe kwa sababu kitendo hicho ni sawa na ukatili
wa kijinsia.
Kauli hiyo
imetolewa leo jijini Dar es Salaam na Mratibu wa Shirika la Wanawake katika
Maendeleo barani Afrika (WiLDAF), Judith Odunga, wakati alipokuwa akitoa taarifa
kuhusu Siku 16 za kupinga Ukatili wa Kijinsia, inayotarajiwa kuanza Novemba 25
hadi Desemba 10.
Alisema hivyo kutokana
na utafiti uliofanywa na Idara ya Takwimu (TDHS), mwaka 2010 na kuonesha kuwa
asilimia 82 ya wanawake wenye umri kati ya miaka 15 hadi 49 walikeketwa.
“ Ukimya katika
masuala ya ukatili wa kijinsia unachangia katika kushamiri kwa vitendo hivi na
hakika bado tuna safari ndefu katika kutokomeza ukatili huu wa
kijinsia,”alisema Judith.
Alisema jamii haina
budi kuongeza nguvu katika mapambano ya kutokomeza vitendo hivyo vya ukatili wa
kijinsia ili kuwa na wanawake wenye afya na familia zenye afya kwa ujumla wake.
Akizungumzia
maadhimisho hayo, alisema Mashirika ya Haki za binadamu , wadau wa maendeleo na
Asasi za Kiraia wanaungana na wadau wengine wa haki za binadamu duniani kupinga
vitendo hivyo aktika siku hizo 16.
Judith, alisema
katika siku hizo za kupinga ukatili wa kijinsia kutakuwa na shughuli na
midahalo mbalimbali ambapo kwa Dar es Salaam yatafanyika katika viwanja vya
Karimjee huku mgeni rasmi akitarajiwa kuwa Waziri Mkuu Mizengo Pinda.
“Mbali na uzinduzi
huo utakaofanyika kitaifa Dar es Salaam, maadhimisho haya pia yatafanyika
katika kanda mbalimbali.
Judith, alizitaja
Kanda hizo kuwa ni Kaskazini, Ziwa, Kati, Kusini na Nyanda za juu Kusini
Magharibi.
Aidha, katika siku
hizo katika maeneo hayo elimu mbalimbali kupitia midahalo, mikutano na semina,
itatolewa na Asasi na mashirika yote katika maeneo husika.
No comments:
Post a Comment