Mwenyekiti wa Vijana CUF Taifa Hamidu Bobali akifafanua
jambo wakati wa mkutano na waandishi wa habari jijini Dar es Salaam,
kuhusu kitendo cha kudhalilishwa kwa Mwenyekiti wa CUF, Prof Ibrahim Lipumba Januari
27 wakati walipokua wanaandamana kwa ajili ya kuwakumbuka wanachama wenzao
ambao waliuawa na kuteswa mwaka 2001 huko Zanzibar. Kulia ni Mwenyekiti wa
Jumuiya ya Vijana CUF, Wilaya ya Kinondoni, Aboubakari Kabambura na Naibu
Katibu Mkuu wa Jumuiya ya Vijana CUF Taifa, Maulid Said. (Picha na Francis Dande)
Na Mwandishi Wetu
JUMUIYA ya Vijana ya Chama cha Wananchi (JUVICUF) wamelaani vikali kitendo
walichokiita cha kinyama kilichofanywa na Jeshi la Polisi kumdhalilisha Mwenyekiti wa CUF Taifa Prof.
Ibrahim Lipumba na Viongozi waandamizi wa Chama wa Ngazi ya Taifa na wilaya.
Akizungumza na Waandishi wa habari jijini Dar es Salaam, Mwenyekiti wa
Vijana CUF, Taifa Hamidu Bobali alisema kuwa kitendo cha kudhalilishwa kwa
Mwenyekiti wao pamoja na wanachama wengine ni unyonyaji wa demokrasia.
Mwenyekiti wa CUF na wanachama wengine walifanyiwa unyanyasaji na
udhalilishaji huo Januari 27 wakati walipokua wanaandamana kwa ajili ya
kuwakumbuka wanachama wenzao ambao waliuawa na kuteswa mwaka 2001 huko
Zanzibar.
Kutokana na hali hiyo Vijana CUF wamemtaka waziri wa Mambo ya ndani ya Nchi, Mathius Chikawe kujiuzuru kutokana na tukio hilo sambamba na kauli waliyoiita
kuwa ya uongo aliyoitoa bungeni.
Jumuiya hiyo imeazimia kuandaa maandamano makubwa ya kulaani vitendo vya
ukiukwaji wa haki za binadamu zinazofanywa na Serikali ya CCM kupitia Jeshi
lake.
Bobali alisema kuwa wanamtaka Mkuu wa Jeshi la Polisi IGP Ernest Mangu
kuona aibu na na kutokubali kuacha wananchi waendelee kuliona jeshi hilo kuwa
limekosa watu wanaoweza kujenga hoja mbele ya umma.
Katika hatua nyingine wameitaka Serikali izifute kesi zote zilizotokana na
tukio hilo la Januari 27 mwaka huu.
"IGP akanushe taarifa ambayo JUVICUF tunaiona ni kauli ya kitoto na
haikupaswa kutolewa na kiongozi mkubwa kama kama Chagonja ameudhihirishia Umma
kuwa Jeshi la Polisi lilikosa sababu ya kuzia maandamano ya CUF badala yake
bila kuona aibu anaibuka na hoja za kitoto zilizokosa mashiko,alisema Bobali".
Alisema hoja ya kuibiwa silaha kwenye kituo cha Polisi Ikwiriri hakina
mahusiano yeyote na kufanyika kwa maandamano CUF na isitoshe CCM wameandaa
maandamano Songea katika kuazimisha tarehe ya kuanzishwa kwa CCM wakiwa
wamesafiri wajumbe wa chama hicho hadi Songea.
Vijana hao walitoa onyo kwa viongozu wa CCM juu ya kuamrishwa kuzalilishwa
kwa viongozi wa CUF na kwamba hawatokaa kimya katika kujibu mapigo juu ya
viongozi wa CCM.
No comments:
Post a Comment