Wachezaji wa Azam FC wakishangilia ushindi wa timu yao baada
ya kuifunga El-Merreikh ya Sudan mabao 2-0 katika mechi ya kwanza ya hatua ya
awali ya Ligi ya Mabingwa Afrika iliyochezwa kwenye Uwanja wa Azam Complex
jijini Dar es Salaam. (Na Mpiga Picha Wetu)
Na Mwandishi Wetu
TIMU ya Azam FC leo imeanza vizuri kampeni ya michuano ya
Ligi ya Mabingwa Afrika baada ya kuwachapa El Merreikh ya Sudan mabao 2-0,
katika mechi ya kwanza kwenye hatua ya awali iliyochezwa Uwanja wa Azam Complex,
jijini Dar es Salaam.
Azam walipata bao la kwanza katika dakika ya nane likifungwa
na nyota wake wa kimataifa wa Burundi, Didier Kavumbagu, nyota aliyetua msimu
huu katika timu hiyo akitokea Yanga.
Licha ya El Merreikh kucharuka kutaka kusawazisha bao hilo,
ukuta wa Azam ulikuwa imara kuokoa hatari zote na hadi mapumziko, Azam walikuwa
mbele kwa bao hilo moja.
Hata hivyo, licha ya kumaliza kipindi cha kwanza wakiwa
nyuma kwa bao hilo moja, El Merreikh, walionesha uwezo mkubwa kiuchezaji na
kama wangekuwa makini, wangeweza kwenda mapumziko wakiwa na bao.
Kipindi cha pili, kiliendelea kuwa kizuri kwa Azam kwani
walionekana wazi kung’ara na katika dakika ya 77, John Boco ‘Adebayor’
aliyeingia kuchukua nafasi ya Kipre Tchetche, aliifungia timu yake bao la pili.
Boco akigusa mpira kwa mara ya kwanza tangu aingie, alifunga
bao hilo kwa kichwa kwa mpira ulitokana na mpira wa kurushwa kabla ya kumkuta Erasto
Nyoni aliyetoa pasi kwa mfungaji.
Bao hilo liliwazindua wageni El Merreikh kwa kuzidi
kulisakama lango la Azam, lakini hadi filimbi ya mwisho, walitoka uwanjani
wakiwa wamelala kwa mabao 2-0.
Ni ushindi uliowaweka Azam katika nafasi nzuri ya kuvuka
raundi ya awali ya michuano hiyo kwani sasa watahitaji walau sare tu
kuwang’oa wakali hao wa Sudan katika
michuano hiyo.
No comments:
Post a Comment