February 18, 2015

RAIS KIKWETE APANGUA WAKUU WA WILAYA

RAIS Jakaya Kikwete amefanya mabadiliko ya wakuu wa wilaya kwa kuingiza sura mpya 27, kuwatema 12 na kuwabadilisha vituo vya kazi 64.

Hata hivyo mabadiliko hayo yanahusishwa na wachambuzi wa kisiasa kama mkakati wa kukiimarisha Chama Cha Mapinduzi (CCM), wakati huu wa kuelekea Uchaguzi Mkuu wa Oktoba mwaka huu.

Katika panga, pangua hiyo, kambi ya Edward Lowassa, ambaye anatajwa kuwania urais kupitia CCM, ndiyo imeathiriwa na mabadiliko hayo kutokana na wapambe wake kadhaa kuachwa huku wale wanaompinga wakichanua.    

Akitangaza mabadiliko hayo leo mjini hapa, Waziri Mkuu, Mizengo Pinda, alisema kuwa uteuzi huo umetokana na wakuu wa wilaya watatu kufariki dunia, watano kupandishwa kuwa wakuu wa mikoa na saba kupangiwa majukumu mengine.

Pia wamo 12 ambao uteuzi wao umetenguliwa na katika mabadiliko hayo, rais amewateua wakuu wapya 27 ili kujaza nafasi hizo wazi. Aidha, wakuu 64 wamebadilishwa vituo vya kazi na 42 wameendelea kubaki katika vituo vya sasa.

Wakuu wa wilaya waliofariki dunia ni Kapteni mstaafu James Yamungu, aliyekuwa Serengeti, Anna Magoha wa Urambo na Moshi Chang’a aliyekuwa Kalambo.

Pinda aliwataja wakuu wa wilaya waliopanda vyeo kuwa wakuu wa mikoa na nafasi zao kubaki wazi kuwa ni John Mongela, aliyetoka Arusha kwenda Kagera , Amina Masenza kutoka Ilemela kwenda Iringa, Dk. Ibrahim Msengi, kutoka Wilaya ya Moshi kwenda Katavi, Halima Dendego, aliyekuwa Tanga kwenda Mtwara na Felix Ntibenda kutoka Karatu kwenda Arusha.

Wateule wapya

Waziri Mkuu aliwataja wakuu wapya na vituo vyao kwenye mabano kuwa ni Mariam Mtima (Ruangwa), Dk. Jasmine Tiisike (Mpwapwa), Pololeti Mgema (Nachingwea), Fadhili Nkurlu (Misenyi) na Felix Lyaniva (Rorya).

Wengine ni Fredrick Mwakalebela (Wanging’ombe), ambaye aliwahi kuwa Katibu Mkuu wa Shirikisho la Mpira wa Miguu Tanzania (TFF), Zainab Mbussi (Rungwe), Francis Mwonga (Bahi) na Kanali mstaafu Kimiang’ombe Nzoka (Kiteto).
Wapo pia Husna Msangi (Handeni), Emmanuel Uhaula (Tandahimba), Mboni Mhita (Mufindi), ambaye pia ni Makamu Mwenyekiti wa Jumuiya ya Vijana wa Chama Cha Mapinduzi (CCM), Hashim Mngandilwa (Ngorongoro), Mariam Juma (Lushoto) na Thea Ntara (Kyela).

Pinda aliwataja wengine kuwa ni Ahmad Nammohe (Mbozi), Shaaban Kissu (Kondoa), ambaye pia ni mtangazaji mkongwe wa Shirika la Utangazaji la Taifa (TBC), Kamanda mstaafu wa Polisi katika mikoa ya Mbeya, Dodoma na Mtwara, Zelote Stephen, ambaye anakuwa mkuu wa Wilaya ya Musoma.

Wateule wengine ni Pili Moshi (Kwimba), Mahmoud Kambona (Simanjiro), Glorius Luoga (Tarime), Zainab Telack (Sengerema), Bernard Nduta (Masasi), Zuhura Ally (Uyui), Mwajuma Nyiruka (Misungwi), Maftah Mohamed (Serengeti) na Katibu wa Uhamasishaji na Chipukizi wa (UVCCM), Paulo Makonda, ambaye anakwenda Wilaya ya Kinondoni jijini Dar es Salaam.

Makonda ni mwanasiasa kijana ambaye hivi karibuni amekuwa kwenye mvutano na baadhi ya wenyeviti wa mikoa wa CCM wanaotajwa kuwa wafuasi wa Lowassa, akidaiwa kuwatuhumu kwamba wanatumika kukivuruga chama.

Majukumu mengine

Katika orodha hiyo, wapo wakuu wa wilaya walioachwa kwa ahadi ya kupangiwa majukumu mengine, ambao ni Brigedia Jenerali mstaafu Cosmas Kayombo (Simanjiro), Kanali mstaafu Ngemela Lubinga (Mlele), Juma Madaha (Ludewa), Mercy Emmanuel (Mkuranga), Ahmed Kipozi (Bagamoyo), Mrisho Gambo (Korogwe) na Elinas Pallangyo (Rombo).

Waliotupwa

Kwa mijibu wa taarifa hiyo ya Pinda, wakuu wa wilaya waliotenguliwa uteuzi wao kutokana na sababu za umri, kiafya na nyinginezo ni James ole Millya, aliyekuwa Longido, Elias Wawa Lali (Ngorongoro), Alfred Msovella (Kongwa) na Dany Makanga (Kasulu).

Wengine ni Fatma Kimario (Kisarawe), ambaye zamani alihamishwa kutoka Igunga baada ya kushambuliwa katika vurugu dhidi ya wafuasi wa Chadema katika uchaguzi mdogo wa Igunga mwaka 2011.

Wapo pia Elibariki Kingu (Igunga), Dk. Leticia Warioba (Iringa), Evarista Kalalu (Mufindi), Abihudi Saideya (Momba), Khalid Mandia (Babati), Elias Goroi Boe Boe Goroi (Rorya) na Martha Umbula (Kiteto), ambaye amekuwa akilalamikiwa kuchochea mgogoro wa ardhi baina ya wakulima na wafugaji wilayani humo.

 Majina ya wakuu wa wilaya waliobadilishwa vituo vya kazi na wale waliobaki kwenye vituo vyao vya zamani, yamechapishwa ukurasa wa nane.

No comments:

Post a Comment

Pages