RAIS Jakaya Kikwete amefanya mabadiliko ya wakuu wa wilaya
kwa kuingiza sura mpya 27, kuwatema 12 na kuwabadilisha vituo vya kazi 64.
Hata hivyo mabadiliko hayo yanahusishwa
na wachambuzi wa kisiasa kama mkakati wa kukiimarisha Chama Cha Mapinduzi
(CCM), wakati huu wa kuelekea Uchaguzi Mkuu wa Oktoba mwaka huu.
Katika panga, pangua hiyo,
kambi ya Edward Lowassa, ambaye anatajwa kuwania urais kupitia CCM, ndiyo
imeathiriwa na mabadiliko hayo kutokana na wapambe wake kadhaa kuachwa huku
wale wanaompinga wakichanua.
Akitangaza mabadiliko hayo leo mjini hapa, Waziri Mkuu, Mizengo Pinda, alisema kuwa uteuzi huo umetokana na
wakuu wa wilaya watatu kufariki dunia, watano kupandishwa kuwa wakuu wa mikoa
na saba kupangiwa majukumu mengine.
Pia wamo 12 ambao uteuzi wao
umetenguliwa na katika
mabadiliko hayo, rais amewateua wakuu wapya 27 ili kujaza nafasi hizo wazi.
Aidha, wakuu 64 wamebadilishwa vituo vya kazi na 42 wameendelea kubaki katika
vituo vya sasa.
Wakuu
wa wilaya waliofariki dunia ni Kapteni mstaafu James Yamungu, aliyekuwa
Serengeti, Anna Magoha wa Urambo na Moshi Chang’a aliyekuwa Kalambo.
Pinda aliwataja wakuu wa
wilaya waliopanda vyeo kuwa wakuu wa mikoa na nafasi zao kubaki wazi kuwa ni John Mongela, aliyetoka
Arusha kwenda Kagera , Amina Masenza kutoka Ilemela kwenda Iringa, Dk. Ibrahim
Msengi, kutoka Wilaya ya Moshi kwenda Katavi, Halima Dendego, aliyekuwa Tanga
kwenda Mtwara na Felix Ntibenda kutoka Karatu kwenda Arusha.
Wateule wapya
Waziri
Mkuu aliwataja wakuu wapya na vituo vyao kwenye mabano kuwa ni Mariam Mtima
(Ruangwa), Dk. Jasmine Tiisike (Mpwapwa), Pololeti Mgema (Nachingwea), Fadhili
Nkurlu (Misenyi) na Felix Lyaniva (Rorya).
Wengine
ni Fredrick Mwakalebela (Wanging’ombe), ambaye aliwahi kuwa Katibu Mkuu wa
Shirikisho la Mpira wa Miguu Tanzania (TFF), Zainab Mbussi (Rungwe), Francis
Mwonga (Bahi) na Kanali mstaafu Kimiang’ombe Nzoka (Kiteto).
Wapo
pia Husna Msangi (Handeni), Emmanuel Uhaula (Tandahimba), Mboni Mhita (Mufindi),
ambaye pia ni Makamu Mwenyekiti wa Jumuiya ya Vijana wa Chama Cha Mapinduzi
(CCM), Hashim Mngandilwa (Ngorongoro), Mariam Juma (Lushoto) na Thea Ntara (Kyela).
Pinda
aliwataja wengine kuwa ni Ahmad Nammohe (Mbozi), Shaaban Kissu (Kondoa), ambaye
pia ni mtangazaji mkongwe wa Shirika la Utangazaji la Taifa (TBC), Kamanda
mstaafu wa Polisi katika mikoa ya Mbeya, Dodoma na Mtwara, Zelote Stephen,
ambaye anakuwa mkuu wa Wilaya ya Musoma.
Wateule
wengine ni Pili Moshi (Kwimba), Mahmoud Kambona (Simanjiro), Glorius Luoga (Tarime),
Zainab Telack (Sengerema), Bernard Nduta (Masasi), Zuhura Ally (Uyui), Mwajuma
Nyiruka (Misungwi), Maftah Mohamed (Serengeti) na Katibu wa Uhamasishaji na
Chipukizi wa (UVCCM), Paulo Makonda, ambaye anakwenda Wilaya ya Kinondoni
jijini Dar es Salaam.
Makonda
ni mwanasiasa kijana ambaye hivi karibuni amekuwa kwenye mvutano na baadhi ya
wenyeviti wa mikoa wa CCM wanaotajwa kuwa wafuasi wa Lowassa, akidaiwa kuwatuhumu
kwamba wanatumika kukivuruga chama.
Majukumu mengine
Katika
orodha hiyo, wapo wakuu wa wilaya walioachwa kwa ahadi ya kupangiwa majukumu
mengine, ambao ni Brigedia Jenerali mstaafu Cosmas Kayombo (Simanjiro), Kanali
mstaafu Ngemela Lubinga (Mlele), Juma Madaha (Ludewa), Mercy Emmanuel
(Mkuranga), Ahmed Kipozi (Bagamoyo), Mrisho Gambo (Korogwe) na Elinas Pallangyo
(Rombo).
Waliotupwa
Kwa
mijibu wa taarifa hiyo ya Pinda, wakuu wa wilaya waliotenguliwa uteuzi wao
kutokana na sababu za umri, kiafya na nyinginezo ni James ole Millya, aliyekuwa
Longido, Elias Wawa Lali (Ngorongoro), Alfred Msovella (Kongwa) na Dany Makanga
(Kasulu).
Wengine
ni Fatma Kimario (Kisarawe), ambaye zamani alihamishwa kutoka Igunga baada ya
kushambuliwa katika vurugu dhidi ya wafuasi wa Chadema katika uchaguzi mdogo wa
Igunga mwaka 2011.
Wapo
pia Elibariki Kingu (Igunga), Dk. Leticia Warioba (Iringa), Evarista Kalalu (Mufindi),
Abihudi Saideya (Momba), Khalid Mandia (Babati), Elias Goroi Boe Boe Goroi (Rorya)
na Martha Umbula (Kiteto), ambaye amekuwa akilalamikiwa kuchochea mgogoro wa
ardhi baina ya wakulima na wafugaji wilayani humo.
Majina ya wakuu wa wilaya waliobadilishwa
vituo vya kazi na wale waliobaki kwenye vituo vyao vya zamani, yamechapishwa
ukurasa wa nane.
No comments:
Post a Comment