February 09, 2015

Wadau waomba kurudishwa kituo cha Mwenge

WADAU wa usafiri waliokuwa wakitumia Kituo cha Mabasi (Daladala), Mwenge wameiomba serikali kufungua kituo hicho kilichokuwa kimefungwa Juni mwaka jana, kuhamishia shughuli zake Makumbusho.

Akizungumza kwa niaba ya wenzake, jijini Dar es Salaam Hamza Hassan, alisema kuwa wameamua kuiomba serikali kuchukulia uzito wapeke suala hilo, ambalo walilipenyeza katika kikao kilichofanyika Februari 6 mwaka huu, katika katika Ofisi ya Katibu Mkuu wa Wizara ya  Uchukuzi.

Hamza, alisema kuwa anaamini kikao hicho kilichohudhuriwa na wajumbe kutoka Mamlaka ya Udhibiti wa Usafiri wa Nchi Kavu na Majini (Sumatra), Mkurugenzi wa Halmashauri ya Wilaya ya Kinondoni, Mhandisi Mussa Natty, Wakala wa Barabara Tanzania (Tanroad), Mkuu wa Kikosi cha Usalama Barabarani (RTO) na wadau wengine wa usafiri.

Mwananchi mwingine Kimaza Kileo alitoa wito kwa Waziri Mkuu Mizengo Pinda atoe maelekezo kwa Waziri wa Wizara ya Elimu na Mafunzo ya Ufundi na Ofisi ya Waziri Mkuu (Tamisemi), Hawa Ghasia na Waziri wa Mawasiliano na Uchukuzi Samwel Sita ili wawezeshe kurudishwa kwa kituo hicho.

“Sisi kama Watanzania wengine wakiwamo wagonjwa, watoto, wanafunzi, watu wenye ulemavu, watu wa rika mbalimbali wakimo akina mama wajawazito wamekuwa wkaipata tabu kutembea kutoka Mwenge hadi kituo cha mabasi cha makumbusho kwa kupitia njia ya Ali Hassan Mwinyi au kutoka Mwenge hadi kituo cha mawasiliano cha njia ya Sam Nujoma.

“Miongoni mwa waathirika hao kuna wafanyabiasha wadogo wadogo, wafanyakazi wa serikali na mashirika ya umma, wajasiriamali na hata wafanyakazi wa vyombo vya ulinzi na usalama wenye vyeo vidogo wamo pia,” alisema Kileo.

Mkazi mwingine James Mrema alisema kuwa anatoa wito kwa wahusika kurudisha njia za zamani ili kuwasaidia walala hoi waepukane ulipaji wa nauli mara nne kwa siku kutoka Mwenge hadi Makumbusho na Kariakoo/Posta hadi Mwenge hadi Mawasiliano.

Mkurugenzi Natty, alipotafutwa kuthibitisha hilo, alikiri kuwa yeye na wadau hao walikutana wizarani kwa ajili ya kujadili maombi yao ambayo wameshauriwa kuyapeleka mkoani.

“Tunatarajia kuwa yatafanyiwa kazi katika wiki hii inayoanza leo (Jumatatu),”alisema Natty.

No comments:

Post a Comment

Pages