MWANAMUZIKI wa nyimbo za asili na
mtayarishaji wa vipindi vya radio, Chigwele Che Mundugwao, amefariki dunia leo
saa moja asubuhi, akiwa katika Hospitali ya Taifa ya Muhimbili alikokuwa akitibiwa
wakati akishikiliwa na Jeshi la Magereza.
Che Mundugwao (48), alikuwa
akiishi gerezani kwa sababu alikuwa akikabiliwa na kesi ya wizi wa Pasi za
kusafiria (pasipoti), mali ya serikali tangu aliposhitakiwa rasmi Katika
Mahakama ya Hakimu Mkazi Kisutu Dar es Salaam, Juni 2, 2013 na wenzake.
Kwa mujibu wa Makamu wa Rais
wa Shirikisho la Muziki Tanzania, Samuel Mbwana, alithibitisha kutokea kwa kifo
cha Che Mundugwao, na kusema msiba uko Tegeta Azania kwa kaka wa marehemu, na
kwamba atazikwa saa 10 alasiri.
“Ni
kweli Chemundugwao amefariki na msiba uko Tegeta Azania kwa kaka wa marehemu. Familia
na kamati ya mazishi ziko katika majadiliano na hakuna uamuzi uliofikiwa wa
makaburi gani atazikiwa, ingawa imekubaliwa azikwe Dar,” alisema Mwana.
Che
Mundugwao, Ofisa Manunuzi wa Idara ya Uhamiaji, Shemweta Kilwasha (33),
Mhandisi wa Idara ya Zimamoto na Ukoaji, Keneth Pius 39 na mfanyabiashara, Ally
Jabir ( 36), walifikishwa katika Mahakama ya Hakimu Mkazi Kisutu, wakikabiliwa
na jumla ya mashitaka manne likiwemo kosa la wizi wa jumla ya Pasipoti 26.
Katika
kesi hiyo, makosa waliyokuwa wakishitakiwa nayo yalikuwa na dhamana kwa mujibu
wa Sheria, ingawa Mkurugenzi wa Mashitaka (DPP), kwa mamlaka aliyonayo, ana haki
kuzuia dhamana, mamlaka iliyomlazimu Che Mundugwao kusota mahabusu.
No comments:
Post a Comment