April 07, 2015

POLISI KWA KUSHIRIKIANA NA ASKARI WA JIJI WAWATISHIA WAANDISHI KWA BASTOLA

 Askari wa jiji wakishirikiana na Polisi kumpandisha kwa nguvu katika gari mfanyabiashara wa kuuza nguo katika Mtaa wa Mkwepu - Posta Mpya, jijini Dar es Salaam leo, kitendo ambacho kimelaaniwa na watu walioshuhudia tukio hilo kutokana na mmoja wa askari hao kuwatishia kwa bastola waandishi wa habari wa gazeti la Tanzania Daima. (Picha na Loveness Bernard).
 Mmoja wa askari aliyekuwa katika gari wanalotumia mgambo wa jiji kwa kushirikia na askari Polisi akiwa ameshika bastola aliyoitumia kuwatishia waandishi wa habari wa gazeti la Tanzania Daima ambao walikuwa wakishuhudia unyanyasanji uliokuwa ukifanywa na askari hao kwa wauza nguo za mtumba katika mtaa wa Mkwepu.

Na MWANDISHI WETU

VITENDO vya kikatili vya kupigwa na kunyang’anya mali za wafanyabiashara mbalimbali kwa kisingizio cha kusafisha jiji na kugawana badala ya kupeleka kunakoruhusiwa vimezidi kujitokeza jijini Dar es Salaam.

WAZIRI Mkuu, Mizengo Pinda aliwahi kuagiza kuwa wakuu wa mikoa na wilaya kukaa na wafanyabiashara na kuangalia njia nzuri ya kufanya biashara ili kuondoa vurugu baina yao na vijana.
 
Pinda aliyasema hayo Januaari mwaka huu katika kipindi cha maswali ya papo kwa hapo kwa Waziri Mkuu alipojibu swali la Mbunge wa Ilala, Iddi Zungu (CCM) aliyetaka kujua kauli ya Serikali kuhusu polisi na wanamgambo wanaotumia nafasi ya kusafisha jiji kuwanyanyasa wafanyabiashara na kugawana mali zao.
 
Amesema yeye binafsi alitumiwa picha ya watendaji hao wakigawana mali walizowanyang’anya wafanyabiashara wakiwamo mamalishe, jambo ambalo ni kuwanyanyasa na kuwarudisha nyuma kimaendeleo.
 
Waziri Mkuu alikemea kitendo cha watendaji wa jiji na mikoa kutumia kusafisha jiji kunyanyasa wananchi.
 
Hivyo aliagiza wakuu wa wilaya na mikoa kukaa na wafanyabiashara ndogo na kupanga jinsi ya kuendesha biashara kistaarabu ikiwa ni pamoja na kupanga masoko ya jioni na Jumapili ili wafanye biashara muda mfupi na kuondoka.

Wakati Pinda akiagiza hayo Jeshi la Polisi wakishirikiana na mgambo katika mtaa wa Mkwepu na Makunganya jijini leo, walitembeza kipigo kwa wamachinga kwa madai kuwa walikuwa wakifanya biashara katika maeneo yasiyo rasmi.

Baadhi ya watu walioshuhudia askari hao wakiwapiga wamachinga hao walilaani kitendo hicho cha kikatii kutokana na wamachinga hao kutii sheria kila walipoelekezwa.

''Mmoja wa mashuhuda wa tukio hilo alisema askari hao waliyokuwa wameshika bastola na bunduki waliwavamia wafanyabiashara hao na kuanza kukusanya bidhaa zao na kuzipakiza katika gari bila ya kuziorodhesha kama inavyotakiwa''.

Mashuhuda hao walisema baada ya kuona vitendo hivyo vya kikatili walianza kuwazomea askari hao ndipo ikasikika kauli ya mmoja wa askari akimuelekeza kuwa apige risasi ili kuwanyamazisha wasizomee.

Hata hivyo, askari aliyekuwa akielekezwa alibaki kuhangaika akiwatafuta watu waliokuwa wakizomea kwani hakuweza kuwaona kwa vile walikuwa wakishuhudia tukio hilo wakiwa gorofani.

Sisi tukio lile lilikuwa halituhusu lakini kilichotukera ni kuona askari ambaye anategemewa kuwa  mlinzi wa amani leo yeye ndio anakuwa wakwanza kuvunja amani kwa kuwapora wananchi mali zao tena kwa kutumia vitisho vya silaha na kipigo bila huruma,”alisema mmoja wa mashuhuda hao.

Mashuhuda hao wametoa rai kwa serikali kuwa makini na vitendo vinavyofanywa na askari pindi wanapokuwa kazini kwa baadhi yao siyo waaminifu, vitendo hivyo vikiachwa viendelee uhusiano kati ya raia wao utakuwa mbaya.

No comments:

Post a Comment

Pages