Askari wa jiji wakishirikiana na Polisi kumpandisha kwa
nguvu katika gari mfanyabiashara wa kuuza nguo katika Mtaa wa Mkwepu - Posta
Mpya, jijini Dar es Salaam leo, kitendo ambacho kimelaaniwa na watu
walioshuhudia tukio hilo kutokana na mmoja wa askari hao kuwatishia kwa bastola
waandishi wa habari wa gazeti la Tanzania Daima. (Picha na Loveness Bernard).
Mmoja wa askari aliyekuwa katika gari wanalotumia mgambo wa jiji kwa kushirikia na askari Polisi akiwa ameshika bastola aliyoitumia kuwatishia waandishi wa habari wa gazeti la Tanzania Daima ambao walikuwa wakishuhudia unyanyasanji uliokuwa ukifanywa na askari hao kwa wauza nguo za mtumba katika mtaa wa Mkwepu.
Na MWANDISHI WETU
VITENDO vya kikatili vya kupigwa na kunyang’anya mali za
wafanyabiashara mbalimbali kwa kisingizio cha kusafisha jiji na kugawana badala
ya kupeleka kunakoruhusiwa vimezidi kujitokeza jijini Dar es Salaam.
WAZIRI
Mkuu, Mizengo Pinda aliwahi kuagiza kuwa wakuu wa mikoa na wilaya kukaa na
wafanyabiashara na kuangalia njia nzuri ya kufanya biashara ili kuondoa vurugu
baina yao na vijana.
Pinda
aliyasema hayo Januaari mwaka huu katika kipindi cha maswali ya papo kwa hapo
kwa Waziri Mkuu alipojibu swali la Mbunge wa Ilala, Iddi Zungu (CCM) aliyetaka
kujua kauli ya Serikali kuhusu polisi na wanamgambo wanaotumia nafasi ya
kusafisha jiji kuwanyanyasa wafanyabiashara na kugawana mali zao.
Amesema
yeye binafsi alitumiwa picha ya watendaji hao wakigawana mali walizowanyang’anya
wafanyabiashara wakiwamo mamalishe, jambo ambalo ni kuwanyanyasa na kuwarudisha
nyuma kimaendeleo.
Waziri
Mkuu alikemea kitendo cha watendaji wa jiji na mikoa kutumia kusafisha jiji
kunyanyasa wananchi.
Hivyo
aliagiza wakuu wa wilaya na mikoa kukaa na wafanyabiashara ndogo na kupanga
jinsi ya kuendesha biashara kistaarabu ikiwa ni pamoja na kupanga masoko ya
jioni na Jumapili ili wafanye biashara muda mfupi na kuondoka.
Wakati Pinda akiagiza hayo Jeshi la Polisi wakishirikiana
na mgambo katika mtaa wa Mkwepu na Makunganya jijini leo, walitembeza
kipigo kwa wamachinga kwa madai kuwa walikuwa wakifanya biashara katika maeneo
yasiyo rasmi.
Baadhi ya watu walioshuhudia askari hao wakiwapiga
wamachinga hao walilaani kitendo hicho cha kikatii kutokana na wamachinga hao kutii sheria kila walipoelekezwa.
''Mmoja wa mashuhuda wa tukio hilo alisema askari hao
waliyokuwa wameshika bastola na bunduki waliwavamia wafanyabiashara hao na
kuanza kukusanya bidhaa zao na kuzipakiza katika gari bila ya kuziorodhesha
kama inavyotakiwa''.
Mashuhuda hao walisema baada ya kuona vitendo hivyo vya
kikatili walianza kuwazomea askari hao ndipo ikasikika kauli ya mmoja wa askari
akimuelekeza kuwa apige risasi ili kuwanyamazisha wasizomee.
Hata hivyo, askari aliyekuwa akielekezwa alibaki
kuhangaika akiwatafuta watu waliokuwa wakizomea kwani hakuweza kuwaona kwa vile
walikuwa wakishuhudia tukio hilo wakiwa gorofani.
“Sisi tukio lile lilikuwa halituhusu lakini kilichotukera
ni kuona askari ambaye anategemewa kuwa
mlinzi wa amani leo yeye ndio anakuwa wakwanza kuvunja amani kwa
kuwapora wananchi mali zao tena kwa kutumia vitisho vya silaha na kipigo bila
huruma,”alisema mmoja wa mashuhuda hao.
Mashuhuda hao wametoa rai kwa serikali kuwa makini na
vitendo vinavyofanywa na askari pindi wanapokuwa kazini kwa baadhi yao siyo
waaminifu, vitendo hivyo vikiachwa viendelee uhusiano kati ya raia wao utakuwa
mbaya.
No comments:
Post a Comment