Na Bryceson Mathias, Morogoro
CHAMA cha Demokrasia na Maendeleo
(Chadema), kimempasha na kumjibu mgombea wa Chama Cha Mapinduzi (CCM), John
Pombe Magufuli, kwamba CCM imemtanguliza shetani badala ya Mungu, ndiyo maana
inashindwa kukomesha mauaji ya wakulima na wafugaji Mvomero.
Katibu wa Chadema Mvomero, Ramadhani Mrisho, alimnanga Magufuli akisema: “Magufuli
alikuwa kwenye Baraza la Mawaziri kwa miaka 10, lakini hakumtanguliza Mungu ili
ampe hekima ya kumshauri Rais Jakaya
Kikwete na CCM wakomeshe mauaji hayo na badala yake yanaendelea hadi leo.”
Alisema CCM na Magufuli wanashindwa
kuelewa kuwa mgogoro wa wakulima na wafugaji unaosababisha, mauaji katika bonde la mpunga la Mgongola na Mbigiri na
Mabwegere, Kilosa, unasababishwa na Wana-CCM wanaotaka kuhodhi kwa nguvu maeneo
ya wakulima, hivyo mchawi hawezi kujiroga mwenyewe.
Hata hivyo Mrisho amemnyooshea Magufuli
kidole akisema: “CCM imemtanguliza shetani si kwa mauaji ya wakulima na wafugaji
tu, bali hata kwa wakulima wadogo wa miwa Mtibwa, wafanyakazi wa Kiwanda cha
Sukari Mtibwa, wanaodhulumiwa haki zao (mishahara na malipo mengine), tangu kiwanda
hicho kibinafsishwe, huku serikali na CCM iko kimya, ikikumbatia maovu.
Hivyo Mrisho amedai, kama Magufuli
atakuwa rais kwa goli la mkono, basi asipotazama upya, atakuwa akilinda miradi
ya wenye uwezo, waliojimilikisha ardhi na kujibinafsisha viwanda, kikiwemo
Kiwanda cha Sukari Mtibwa, kinachodhulumu wakulima na wafanyakazi wake,
kikidaiwa kuhusishwa na kubebwa na rais mmoja mstaafu.
Kauli ya Chadema Mvomero ilifuatia hotuba
ya Magufuli aliyejitambulisha jana mkoani Morogoro ambapo alisema, kuhusu mgogoro
na mauaji ya wakulima na wafugaji wilayani Mvomero, wananchi na viongozi,
wamtangulize Munngu na kuwa na utu, jambo ambalo Chadema wanasema:
“Mungu katika 1 Timotheo 5:8 anasema:
‘Lakini Mtu yeyote asiyewatunza walio wake (wananchi), yaani wale wa nyumbani
mwake hasa, ameikana imani, tena ni mbaya kuliko mtu asiyeamini…’”
Hivyo CCM haiwajali watu wake, ni mbaya
kuliko wapinzani, alisema Martha Kimbisa mkazi wa Dumila aliyehudhuria
mkutano wa Magufuli.
No comments:
Post a Comment