HABARI MSETO (HEADER)


Breaking

July 25, 2015

NANI NI NANI KATI YA YANGA NA KHARTOUM JUMAPILI?

Hatua ya makundi ya michuano ya Vilabu Bingwa Afrika Mashariki na Kati (Kagame Cup 2015) inatarajiwa kukamilika kesho jumapili kwa michezo miwili kupigwa uwanja wa Taifa jijini Dar es salaam, huku macho na masikio ya wapenzi wa soka yakiwa katika mchezo kati ya Yanga SC dhidi ya Kahrtoum ya Sudan.

Mchezo huo unatarajiwa kuanza saa 10 kamili jioni, ambapo Yanga SC watashuka dimbani kusaka ushindi wake wa tatu mfululizo katika michuano hiyo, hali kadhalika timu ya Khartoum ikihitaji ushindi wake wa tatu katika mechi hiyo inayosuburiwa kwa hamu kubwa.

Kuelekea katika mchezo huo unaotarajiwa kuwa wa vuta ni kuvute kufuatia timu ya Yanga SC kuhitaji ushindi katika mchezo huo ili kujiweka katika nafasi nzuri ya kuongoza kundi lake, huku pia Khartoum wakihitaji ushindi katika mchezo huo ili kuweza kuongoza kundi A.

Utamu wa mchezo huo unaletwa na makocha wa timu hizo mbili, Hans Van der Pluijm wa Yanga na James Kwesi Appiah wa Khartoum ambao wote wamewahi kufanya kazi nchini Ghana kwa vipindi tofauti.

Hans ambaye ametwaa Ubingwa wa Ligi Kuu ya Vodacom Tanznaia msimu huu, anasifika kwa kucheza soka safi la kasi na kushambulia muda wote, huku akiwa na mafanikiko nchini Ghana baada ya kuingia hatua ya robo fainali ya Ligi ya Mabingwa Afrika na timu ya Berekum Chelsea miaka miwili iliyopita.

Kwa upande wa James Appiah alikuwa kocha mkuu wa timu ya Taifa ya Ghana, ambapo alikua kocha wa kwanza mwafrika kuipeleka timu ya Afrika katika fainali za Kombe la Dunia zilizofanyika nchini Brazil mwaka 2014.

Licha ya kufuzu kwa fainali za kombe la Dunia, Appiah pia aliwahi kuichezea timu ya Taifa ya Ghana kwa miaka 7 akiwa nahodha, pia aliiwezesha timu ya Vijana ya Ghana chini ya miaka 23 kufuzu kwa fainali za Michezo ya Afrika na kutwaa Ubingwa huo mwaka 2011.

Katika kikosi chake cha Khartoum kinachoshiriki michuano ya Kagame, Appiah amejumuisha wachezaji wa kimataifa kutoka nchini Cameroon na Ghana, na malengo yake ni kutwaa Ubingwa wa Kagame Cup kwa mara ya kwanza.

Mpaka sasa Khartoum inaongoza kundi A ikiwa na pointi 7 sawa na Gor Mahia lakini Wasudani hao wakiwa juu kwa tofauti ya magoli ya kufunga na kufungwa, huku Yanga wakishika nafasi ya tatu wakiwa na pointi sita.

Kabla ya mchezo huo kati ya Yanga SC dhidi ya Khartoum kutakua na mchezo wa kwanza utakaoanza majira ya saa 8 kamili mchana kati ya Gor Mahia ya Kenya dhidi ya  Telecom ya Djibout.

Mpaka sasa timu zilizofuzu hatua ya robo fainali ni Khartoum, Gor Mahia na Yanga kutoka kundi A, huku APR na Al Shandy zikitoka kundi B, na Azam FC ikiwa timu ya kwanza kufuzu kutoka kundi C, na timu mbili kati ya Adama City, KCCA na Malakia zitaingia hatua ya robo ya fainali.

Hatua ya robo fainali ya michuano ya kombe la Kagame itachezwa Jumanne, Julai 28 na Jumatano Julai 29 katika uwanja wa Taifa jijini Dar es salaam.



LOC YAWASILISHA MALALAMIKO CECAFA
Kamati ya ndani ya uendeshaji wa mashindao ya kombe la Kagame nchini Tanzania (LOC) imewasilisha malalamiko kwa katibu mkuu wa CECAFA, Nicholaus Musonye juu ya vitendo vya utovu wa nidhamu viliyoonyeshwa na timu ya Gor Mahia.

Katika mchezo wa kwanza uliochezwa tarehe 18 Julai, Kocha mkuu wa Gor Mahia Frank Nuttal alionyesha inshala ya matusi kwa kidole, jambo liliopelekea kuzua zogo na washabiki wa mpira waliokuwepo uwanjani kushuhudia mchezo huo.

Wakati wa mapumziko pia timu ya Gor Mahia hawakupita mlango mkubwa wa kuingilia vyumbani, badala yake walitumia kuingilia na kutokea upande wa Kaskazini mwa uwanja wa Taifa, mlango ambao ni maalumu kwa wafanyakazi wa kituo cha runinga cha Supersport.

Lakini katika hali ya kushangaza jana katika mchezo wake dhidi ya Khartoum walirudia kutumia mlango ule ule kwa kuvunja kitasa cha mlango ili waweze kupita kuingia uwanjani kitu ambacho ni kinyume na kanuni na utaratibu wa mashindano.

LOC imeitaka CECAFA kuichukulia hatua kali timu ya Gor Mahia kutokana na vitendo hivyo ilivyovifanya vya kuharibu miundombinu ya uwanja wa Taifa, ambao unatumika kwa ajili ya michezo mbalimbali ya kimataifa.


IMETOLEWA NA SHIRIKISHO LA MPIRA WA MIGUU TANZANIA (TFF)

No comments:

Post a Comment

Pages