Na Bryceson Mathias, Mvomero
KATIBU wa Chama cha Demokrasia na Maendeleo (Chadema) Wilaya ya
Mvomero, Ramadhani Mrisho, amewataka washindi wa kura za maoni ndani ya Chama cha
Demokrasia na Maendeleo (Chadema), kuwa na kauli njema kwa wanachama wao ili
kuepuka mamluki wanaotumika kuwachafua.
Mrisho alisema hayo kufuatia kuwepo taarifa za wanachama, kutumika
na watia nia walioshindwa katika kinyang’anyiro cha udiwani na ubunge katika
kata na majimbo yao, wanaowashawishi wachovu wa siasa wawashitaki washindi wa udiwani
na ubunge kwa uzushi.
Mrisho alisema amesikitishwa na baadhi ya wanachama na viongozi,
ambao wanatumiwa na wapinzani wa Chadema, wanaotumia muda wao mwingi kutunga
habari za uzushi kwa wanasiasa walioshinda kwenye kata na majimbo ya Chadema
kwa lengo la kuwachafua ili Oktoba 25, maadui wa Umoja wa Katiba ya Wananchi
(UKAWA) washinde.
Mrisho alisema kuwa wapo watu ambao wanakosa sera za kisiasa na
kuamua kuwachafua watu wengine kwa kuwapakazia mambo ambayo hayana kichwa wala
miguu, hivyo Chadema Wilaya ya Mvomero ikiwabaini itawafukuza kwa kufuta taratibu
za chama.
Akizungumzia suala la kujiunga kwa Waziri Mkuu mstaafu, Edward
Lowasa, katika Chadema, alisema ni dalili nzuri ambazo zinaonyesha CCM imechoka
na inatakiwa iondolewe madarakani kwa njia ya kidemokrasia bila kumwaga damu.
Amesema kutokana na hofu ya viongozi wa CCM kuanza kutengeneza
mikakati ya kutaka kuwadhoofisha Watanzania wapenda maendeleo kwa kutunga uongo
wakiwatumia Wana Chadema dhaifu, alidai kwa sasa wapo viongozi makini ndani ya
Chadema.
“Watanzania naomba msisikilize maneno ya wazushi ambao wameishiwa
sera, hakuna kiongozi makini ambaye anaweza kuondoka Chadema, tunapambana na
adui ambaye ni CCM na ni lazima tumshinde tena kwa kishindo kikubwa,”
alisema Mrisho.
No comments:
Post a Comment