HABARI MSETO (HEADER)


Breaking

August 19, 2015

IRELAND YAWADHAMINI WATANZANIA 14 KWA SHAHADA YA UZAMILI

Balozi wa Ireland nchini Tanzania, Bi. Fionnuala Gilsenan, akitoa hotuba yake wakati wa maonyesho ya sayansi kwa wanafunzi wa sekondari yanayoandaliwa na shirika la YST ambayo pia Ubalozi wake unadhamini kila mwaka.

Na Daniel Mbega

UBALOZI wa Ireland nchini Tanzania, umewapatia scholarship Watanzania 14 ili kusoma kozi mbalimbali za shahada ya uzamili (masters) na huku wanne kati yao wakienda kusoma vyuo vya nje ya nchi hasa University College Dublin, Dublin Institute of Technology na National University of Ireland Maynooth. 

Kwa mujibu wa taarifa kutoka Ubalozi wa Ireland nchini, scholarship hizo zimetolewa na ubalozi huo kama sehemu ya Mpango wa Mafunzo wa Kila Mwaka (Fellowship Training Programme), ambapo wataalamu wanne waliobahatika kwenda ng’ambo watakwenda kusomea kozi za Maendeleo Endelevu (Sustainable Development), Kilimo na Maisha ya Vijijini (Agriculture and Rural Livelihoods), Rasilimali Watu (Human Resource Management), na Immunolojia na Afya ya Binadamu (Immunology and Human Health).

Watanzania wengine 10 wamedhaminiwa kusomea kozi mbalimbali katika vyuo vikuu vya hapa nchini.

Taarifa hiyo inasema, sherehe za kuwapokea wale walihitimu na kuwakabidhi scholarship wale wanaokwenda kuanza, zitafanyika kesho mchana katika ofisi za Ubalozi zilizoko Masaki, jijini Dar es Salaam ambapo Balozi wa Ireland nchini, Fionnuala Gilsenan, ndiye atakayetoa scholarship hizo.

Mpango huo wa Mafunzo wa kila Mwaka, kwa mujibu wa taarifa hiyo, kwa kiasi kikubwa unahusisha Mfuko wa Misaada wa Ireland (Irish Aid) kupitia program ya maendeleo ya Ubalozi huo nchini Tanzania.

Wanufaika wa mpango huo wameteuliwa na washirika wa maendeleo wa Ireland nchini Tanzania, zikiwemo wizara mbalimbali za Serikali, halmashauri za wilaya na mashirika yasiyo ya kiserikali, ambayo shughuli zao zinawiana na maeneo ya vipaumbele vya Irish Aid, hususan Kilimo, Afya, Lishe na Utawala.

Aidha, wanufaika wote ni watendaji wa kati ambao baada ya kuhitimu masomo yao watarejea kwenye mashirika na taasisi zao kutumia ujuzi walioupata kwa manufaa ya jamii.

“Kwa wanufaika watakaokwenda kusoma nchini Ireland, program inatoa fursa nzuri ya kujifunza katika hadhi ya kimataifa na kunufaika na hazina kubwa ya nyenzo za tafiti zinazotolewa kwenye Vyuo Vikuu na Taasisi za Teknolojia za Ireland,” imeeleza taarifa hiyo.

Ikaongeza: “Inatarajiwa kwamba mafunzo ya wataalamu hawa yatachangia kwa kiasi kikubwa maendeleo ya Tanzania, na kuendelea kuimarisha ushirika wa kielimu baina ya Ireland na Tanzania.”

Ireland, kupitia Mfuko wa Misaada (Irish Aid), imekuwa ikidhamini Mpango huo wa Mafunzo nchini Tanzania kwa miaka 40 sasa ambapo program hiyo imekuwa msingi wa msaada katika kuzijengea uwezo nchi zinazoendelea na inaendana na mkakati wa kupunguza umaskini wa nchi washirika wa Ireland, hasa lengo likiwa kuwapatia wataalamu elimu ya juu ili waendeleze taasisi zao.

Baadhi ya taasisi washirika zitakazonufaika na mpango wa mwaka huu ni pamoja na Wizara ya Kilimo, Chakula na Ushirika, Wizara ya Mifugo na Maendeleo ya Uvuvi, Halmashauri ya Wilaya ya Kigoma, Halmashauri ya Wilaya ya Misenyi, Halmashauri ya Wilaya ya Kondoa, Halmashauri ya Wilaya ya Muheza, Halmashauri ya Wilaya ya Ngorongoro, Taasisi ya Chakula na Lishe, Hospitali ya CCBRT, shirika la Sikika, Mpango wa Maendeleo wa Kinapa (Kinnapa Development Programme), shirika la CARE Tanzania na Taasisi ya Afya Ifakara (IHI).

No comments:

Post a Comment

Pages