August 02, 2015

Taswa FC yashinda 5-3, yaomba udhamini kwa wadau

Mchezaji wa Taswa FC, Shadrack Kilasi akimiliki mpira katika moja ya mechi za timu hiyo mkoani Iringa.

Na Mwandishi wetu

Timu ya soka ya waandishi wa habari za michezo nchini, Taswa FC imeendelea kutamba katika mechi zake za kirafiki baada ya kuisambaratisha timu ya Warioba Veterans mabao 5-3 katika mchezo uliofanyika kwenye uwanja wa Bora, Kijitonyama. 

Taswa FC ambayo inadhaminiwa na Benki ya Posta Tanzania (TPB) ilianza mchezo huo polepole huku wapinzani wao wakiongozwa na Barnaba Emilio na Jerry Mtetema kutawala dakika 10 za mwanzo na kukosa mabao kadhaa. 

Taswa FC chini ya Ali Mkongwe, Majuto “Ronaldo” Omary, Salum Jaba, Julius Kihampa, Athuman Jabir na Khatimu Naheka walianza kulishambulia lango la wapinzani wao na kupata bao la kuongoza katika dakika ya 13 kupitia kwa Julius Kihampa baada ya pasi safi ya Mkongwe.

Bao hilo halikudumu sana na dakika mbili baadaye, Warioba Veterans walisawazisha kupitia wa Barnaba Emilio kwa njia ya penati baada ya Fred “Chuji” Mbembela kucheza faulo ndani ya eneo la hatari. Bao hilo liliwafanya Taswa FC kuongeza mashambulizi na kufuanga bao la pili kupitia kwa Kihampa tena baada ya pasi ya Majuto.  

Warioba ilisawazisha kupitia kwa Mtetema kabla ya Kihampa kufunga bao la tatu kwa Taswa FC na Stanley Abasirim kufunga la nne kufuatia pasi ya Tito Jonathan na Kihampa kufunga la tano dakika ya 78 ya mchezo baada ya pasi safi ya Jabir Johnson. Mtetema alifunga bao la tatu kwa timu yake katika dakika ya 85 ya mchezo.

Mwenyekiti wa Taswa FC, Majuto aliwapongeza wachezaji wake kwa ushindi huo ambao ni chachu kwao kuelekea kushiriki katika bonanza la waandishi wa habari mkoa Arusha Agosti 29 mwaka huu.

Majuto alisema Taswa FC inahitaji msaada wa kifedha na vifaa ili kuweza kufika Arusha na kufanya vyema katika mashindano hayo ya kila mwaka. “Tuna timu nzuri sana ya mpira wa miguu na mpira wa pete, mwanzoni mwa mwaka huu kupitia udhamini wa benki ya Posta Tanzania tulimaliza katika nafasi ya pili mkoani Iringa, tunawaomba wadhamini watusaidie kufikia malengo yetu,” alisema Majuto.

No comments:

Post a Comment

Pages