August 03, 2015

Waziri wa Kikwete akaribishwa Chadema atubu dhambi

Na Bryceson Mathias, Mvomero

BAADA ya Naibu Waziri wa Maji, Amos Makalla, kuangukia pua kwenye uchaguzi wa kura za maoni za Chama Cha Mapinduzi (CCM) Mvomero, Chama cha Demokrasia na Maendeleo (Chadema), kimemkaribisha Makalla kwenye ukombozi, isipokuwa atubu dhambi kwa wananchi.

Akiwa safarini kuelekea kwenye kikao cha Halmashauri Kuu ya Chadema taifa, Katibu wa Chadema Mvomero, Ramadhani Mrisho, amemkaribisha aende Chadema akisema: “Licha ya Makalla kuwapiga mabomu wakati huo, walijua hatatawala milele, hivyo wanamkaribisha kwa sharti la kutubu dhambi alizowafanyia wananchi.

“Tulijua, aliye juu mngoje chini atashuka! Wananchi wa mji mdogo wa Madizini Mtibwa, Mvomero, tulimngoja Makalla chini, hata alipotumia Jeshi la Polisi kutupiga mabomu   tukidai haki ya ushindi wake tata alioupata, tulijua atashuka, maana hata pua  zinaelekea chini.

“Pamoja na kwamba ameangukia pua kwenye uchaguzi wa ubunge ndani ya chama chake, Chadema tunamkaribisha aje atubu dhambi aliyotufanyia, tumsamehe, halafu tushirikiane kwenye mapambano ya kuing’oa CCM Oktoba 25, mwaka huu,” alisema Mrisho.  

Kauli ya Mrisho inakuja baada ya Mbunge wa zamani wa Jimbo la Mvomero, Sadiq Murad, ambaye pia ni Mwekahazina wa CCM wa Wilaya ya Mvomero, kumwangusha Naibu Waziri wa Maji Makalla, katika uchaguzi wa kura za maoni ndani ya chama hicho.

Wadadisi wa siasa wanadai, mbali ya wananchi wa Mvomero kuchoshwa na ahadi za Makalla zisizotekelezeka, jambo jingine lililomwangusha Makalla ni manyanyaso na malipo ya wakulima wadogo wa miwa na wafanyakazi wa Kiwanda cha Sukari Mtibwa, mauaji ya wakulima na wafugaji na maji ambavyo ameshindwa kuvishughulikia. 

Hata hivyo, juhudi za kumpata Makalla ili kuzungumzia kuanguka kwake hazikufanikiwa, lakini alipotafutwa Katibu wake wa Jimbo la Mvomero, Jumanne Kombo, ili azungumzie changamoto za mchakato wa Uchaguzi wa CCM, ziligonga mwamba kutokana na harakati za uchaguzi huo na akipatikana mtahabarishwa.

No comments:

Post a Comment

Pages