Na Bryceson
Mathias, Mvomero
BAADA ya Naibu
Waziri wa Maji, Amos Makalla, kuangukia pua kwenye uchaguzi wa kura za maoni za
Chama Cha Mapinduzi (CCM) Mvomero, Chama cha Demokrasia na Maendeleo (Chadema),
kimemkaribisha Makalla kwenye ukombozi, isipokuwa atubu dhambi kwa wananchi.
Akiwa safarini
kuelekea kwenye kikao cha Halmashauri Kuu ya Chadema taifa, Katibu wa Chadema
Mvomero, Ramadhani Mrisho, amemkaribisha aende Chadema akisema: “Licha ya
Makalla kuwapiga mabomu wakati huo, walijua hatatawala milele, hivyo wanamkaribisha
kwa sharti la kutubu dhambi alizowafanyia wananchi.
“Tulijua, aliye
juu mngoje chini atashuka! Wananchi wa mji mdogo wa Madizini Mtibwa, Mvomero,
tulimngoja Makalla chini, hata alipotumia Jeshi la Polisi kutupiga mabomu tukidai haki ya ushindi wake tata
alioupata, tulijua atashuka, maana hata pua zinaelekea
chini.
“Pamoja na kwamba
ameangukia pua kwenye uchaguzi wa ubunge ndani ya chama chake, Chadema
tunamkaribisha aje atubu dhambi aliyotufanyia, tumsamehe, halafu tushirikiane
kwenye mapambano ya kuing’oa CCM Oktoba 25, mwaka huu,” alisema Mrisho.
Kauli ya Mrisho
inakuja baada ya Mbunge wa zamani wa Jimbo la Mvomero, Sadiq Murad, ambaye pia
ni Mwekahazina wa CCM wa Wilaya ya Mvomero, kumwangusha Naibu Waziri wa Maji
Makalla, katika uchaguzi wa kura za maoni ndani ya chama hicho.
Wadadisi wa siasa
wanadai, mbali ya wananchi wa Mvomero kuchoshwa na ahadi za Makalla
zisizotekelezeka, jambo jingine lililomwangusha Makalla ni manyanyaso na malipo
ya wakulima wadogo wa miwa na wafanyakazi wa Kiwanda cha Sukari Mtibwa, mauaji
ya wakulima na wafugaji na maji ambavyo ameshindwa kuvishughulikia.
Hata hivyo, juhudi
za kumpata Makalla ili kuzungumzia kuanguka kwake hazikufanikiwa, lakini
alipotafutwa Katibu wake wa Jimbo la Mvomero, Jumanne Kombo, ili azungumzie changamoto
za mchakato wa Uchaguzi wa CCM, ziligonga mwamba kutokana na harakati za uchaguzi
huo na akipatikana mtahabarishwa.
No comments:
Post a Comment