HABARI MSETO (HEADER)


Breaking

December 28, 2015

BAKWATA WAMKANA MENEJA SHULE YA EL-HIJRA

DODOMA, Tanzania

KATIBU  Mkuu wa Baraza Kuu la Waislam Tanzania (Bakwata), Seleman Lolila amemkana Meneja wa Shule za El-Hijra Mashaka Kitundu, kwamba amekuwa akimkingia kifua katika matatizo yake na watumishi wenzake.

Lolila alitoa kauli hiyo kwa njia ya simu kwa lengo la kutoa ufafanuzi juu ya malalamiko ya watumishi na walimu wa shule za sekondari za El-Hijra na Jamhuri kwa kutolipwa mishahara na stahiki zao kwa wa kati.

Lolila, alisema hawezi kumkingia kifua Kitundu na wala hahusiki kwa jambo lolote kuhusu madai hayo ya Kitundu.

"Mimi nipo Dar es Salaam Kitundu ndiye anayelipa mishahara sasa mimi nitankingiaje kifua mimi, hebu muuluzeni mwenyewe Kitundu, "alisema Lolila.

Lolila, alifikia hatua hiyo baada ya Kitundu kujigamba mbele ya watumishi wenzake waliyokuwa wakimlalamikia kuhusu kucheleweshewa mishara yao pamoja na stahiki nyingine kwamba waisingemfanya chochote kwa vile yuko karibu na Katibu Mkuu huyo ambaye alidai alikuwa akimlinda na anayeweza kumfukuzisha kazi.

Mvutano huo umekuja mara
baada ya Watumishi wa shule hizo kwa nyakati tofauti kwa kulalamika Kitundu kwamba amekuwa akiwanyanyasa watumishi hao huku akitumia jina la Katibu Mkuu wa Bakwata taifa.

Kutokana na hali hiyo watumishi na walimu wa shule hiyo ya Sekondari za El- Hijra  pamoja na  Jamhuri  ambazo zinamilikiwa na Bakwata, wamemuomba Mufti wa tanzania Sheikh Abubakari Zuberi kumsimamisha kazi Meneja wa shule hizo, Mwashaka Kitundu na ikishindikana  wametishia kugoma.

Watumishi hao wamefikia hatua hiyo kwa madai kwamba hawana imani na mkuu wa shule ya Sekondari ya EL Hijra ambaye pia ni Meneja wa shule ya Hijra na Jamhuri huku pia ni Kaimu Katibu wa Bakwata Mkoa, Kitundu, kutokana na manyanyaso wanayoyapata ikiwa ni pamoja na kutolipwa mishahara yao na stahiki nyingine kwa muda mrefu sasa.

Wakizungumzia adha yanayopata watumishi hao walisema ni kutolipwa mishahara yao huku Meneja huyo akiendelea kujineemesha, kujenga nyumba ya kifahari na kununua magari.
Watumishi hao pamoja na walimu walisema kwamba kwa sasa wana hali mbaya kwani hawajalipwa mishahara yao na pale wanapodai wanapigwa kalenda.

"Tangu mwezi wa saba hadi mwezi huu hatujalipwa mishahara,mara tunalipwa sh.10000 na wengine wanapewa sh.50000 na hatujui ni za nini.

"Mbaya zaidi Meneja Kitundu ametugawa watumishi kuwa wale ambao amewafanya watu wake wa karibu huku wengine akiwa hataki hata kuwasikiliza" alisema mmoja wa watumishi.
Walisema tangu Kitundu awe meneja katika shule hizo  hali ya watumishi imekuwa mbaya lakini jambo la ajabu ni matumizi kuwa makubwa tofauti na kipindi cha nyuma.

"Hivi karibuni alitumia kiasi cha sh.laki 8 kwa wiki kulisha wanafunzi wa Bweni ambao ni kati ya 150 ambapo kawaida wanafunzi hao wa bweni utumia laki 4.5 kwa wiki" walieleza.

Katika msisitizo  watumishi walimuomba Mufti wa Taifa Abbakari Zuberi kumwondoa au kumsimamisha kazi ili uchunguzi ufanyike kubaini ubadhilifu alioufanya kwa muda mfupi tangu afike shuleni hapo.
Katika hatua nyingine watumishi hao walisema Kitundu amekuwa akiwabeza watumishi kwa maelezo kuwa hakuna mtu wa kumfanya lolote kwani yeye anamahusiano makubwa na Katibu mkuu wa Bakwata Taifa,Seleman Lolila.

Hata hivyo watumishi na walimu walisema baada ya kumbana meneja aliwapatia kiwango sawa wote laki moja kama sehemu ya kupunguza ukali wa maisha.

Kwa upande wake Meneja wa shule hizo alipoulizwa juu ya tuhuma hizo alisema suala la mishahara ni tatizo lakini amelazimika kukopa benki na kulipa mishahara.

"Watumishi na walimu walikuwa hawajalipwa mshahara kwa miezi mitatu lakini ni kutokana na ada kuchelewa hivyo nimelazimika kukopa fedha kwa ajili ya kulipa mishahara ya miezi mitatu"alisema Kitundu.

No comments:

Post a Comment

Pages