DAR ES SALAAM, Tanzania
FILAMU ya kiungo Haruna Niyonzima (pichani) na uongozi wa Yanga imefikia mwisho baada ya nyota huyo raia wa Rwanda kuvunjiwa mkataba.
FILAMU ya kiungo Haruna Niyonzima (pichani) na uongozi wa Yanga imefikia mwisho baada ya nyota huyo raia wa Rwanda kuvunjiwa mkataba.
Yanga, mbali ya kuvunja mkataba, pia imemtaka Niyonzima kulipa kiasi cha dola 71,175 za Marekani zaidi ya Sh. Milioni 140.
Klabu hiyo imetoa sharti hilo kwa Niyonzima kwani yeye ndiye aliyeshindwa kuishi na klabu hiyo kwa mujibu wa matakwa ya mkataba baina yao.
Sababu za Yanga kuamua kusitisha mkataba na Niyonzima ni kutokana na kushindwa kuthamini kazi yake na kuonyesha vitendo vya utovu wa nidhamu.
Niyonzima aliingia katika mvutano na Yanga tangu Novemba, baada ya nyota huyo kwenda kwao Rwanda kuichezea timu ya taifa ‘Amavubi’ katika michuano ya Chalenji iliyofanyika Ethiopia kati ya Novemba 21 hadi Desemba 6.
Tatizo baina ya pande hizo mbili lilianza pale nyota huyo aliposhindwa kurejea Yanga kwa wakati licha ya kutakiwa kufanya hivyo mara kadhaa na kibaya zaidi akawa anazima simu.
Nyota huyo baada ya kurejea nchini Desemba 14, aliwakuta wenzake wameanza programu muda mrefu.
Tabia hiyo ya Niyonzima kuchelewa kurudi kila anapokwenda kwao mara kwa mara, safari hii klabu hiyo ikaamua kuchukua uamuzi mgumu katika kulinda nidhamu ya timu.
Akizungumza jijini Dar es Salaam jana, Mkuu wa Idara ya Habari na Mawasiliano wa Yanga, Jerry Muro, alisema wamevunja mkataba huo baada ya Niyonzima kushindwa kutii sheria na taratibu za mkataba wake.
Alisema kiungo huyo atalazimika kuilipa fidia Yanga kwa kuwa amevunja vifungu vya mkataba kwa makusudi, hivyo atalazimika kulipa kiasi hicho kama fidia ya gharama ambazo Yanga imezitumia kumwongeza mkataba ambao ungefikia mwisho mwaka 2017.
“Kutokana na kanuni namba 4 ya FIFA (Shirikisho la Soka la Kimataifa), juu ya kuimarisha mikataba kati ya wachezaji wa kulipwa na klabu, kanuni ya 17 vipengele vya 1, 2, 4 na 5 vinaongelea mambo muhimu kuhusu uvunjaji wa mkataba na mchezaji kulipa gharama kwa klabu,” alisema Muro.
Aliongeza kuwa kutokana na vipengele hivyo, Yanga itapinga usajili wa mchezaji huyo kusajiliwa na timu nyingine kama atakuwa hajalipa fidia hiyo.
Vilevile alisema kuwa Niyonzima amekuwa akikosekana mara kwa mara katika programu za timu, hasa anapokwenda kwao kwa likizo au kuitumikia timu yake ya taifa, pia amekuwa akiondoka bila kutoa taarifa.
Makosa mengine ambayo Niyonzima amekuwa akiyafanya ni kushiriki michuano ambayo si rasmi bila kuruhusiwa na klabu na kuweka masilahi yake mbele kuliko yale ya klabu.
Alisema kwa kipindi kirefu, Niyonzima amekuwa akifanya mambo na kuonyesha tabia ambazo si za kimichezo kiasi cha kuaithiri timu, hivyo Yanga walikuwa wakimvumilia tu.
“Mchezaji huyu ameendelea kurudia mambo haya mara kwa mara, japokuwa klabu ilimpa onyo kwa barua na wakati mwingine kukatwa mshahara...Kwa ufupi tabia zake zimekuwa zikiigharimu timu,” alisisitiza Muro.
Aliongeza kuwa Niyonzima ameonyesha dharau kubwa kwa Kamati ya Nidhamu iliyomtaka awasilishe maelezo yake kimaandishi yaweze kupitiwa, akapuuza agizo hilo.
“Kikao cha Kamati ya Nidhamu na Niyonzima kilichofanyika Desemba 22, alikiri kosa na baadaye kamati ilimuomba kutoa maelezo kwa maandishi kama jinsi alivyojieleza na kuwasilisha siku iliyofuata.
“Kwa bahati mbaya, mchezaji hajawasilisha maelezo yake wala hakutokea kikaoni tena bila taarifa yoyote,” alisema Muro.
Alisema kitendo cha kutotii maagizo hayo ni ukosefu wa nidhamu aliouonyesha kwa uongozi wa Yanga, hivyo klabu haiwezi kukumbatia matendo ya mchezaji huyo kwa kuwa Yanga ni taasisi kongwe na inaendeshwa kwa misingi ya katiba na taratibu zake.
No comments:
Post a Comment