HABARI MSETO (HEADER)


Breaking

April 06, 2016

DK. SHEIN AZIKA SERIKALI YA UMOJA WA KITAIFA ZANZIBAR

Rais wa Zanzibar na Mwenyekiti wa Baraza la Mapinduzi, Dk. Ali Mohamed Shein, akisalimiana na Spika wa Baraza la Wawakilishi, Zubeir Ali Maulid, mara baada ya kuwasili katika viwanja vya jengo la Baraza hilo, Mbweni, nje kidogo ya mji wa Zanzibar ili kuzindua Baraza la Tisa. (Picha na Ikulu).  

TALIB USSI NA MAUWA MUHAMMED, ZANZIBAR

HATIMAYE Rais wa Zanzibar na Mwenyekiti wa Baraza la Mapinduzi, Dk. Ali Muhammed Shein, amesema hakuna uwezekano wa kuunda Serikali ya Umoja wa Kitaifa (SUK) kwa miaka mitano atakayokuwapo madarakani.

Dk. Shein alisema uamuzi wa kukichagua Chama Cha Mapinduzi (CCM) katika uchaguzi wa marudio uliofanyika Machi 20, mwaka huu kwa asilimia 91.4 kumezika Serikali ya Umoja wa Kitaifa (SUK) inayotambuliwa kikatiba.

Kiongozi huyo alisema Katiba ya Zanzibar inaweka wazi kuwa kama kuna chama kingine kitapata asilimia 10 ya kura kinakidhi matakwa ya kuwa kwenye serikali hiyo.

Kauli hiyo aliitoa jana wakati akilizindua na kulihutubia Baraza la Wawakilishi, ambapo alisema uchaguzi wa marejeo, vyama 14 vya siasa vilishiriki na hakukuwa na chama chochote zaidi ya CCM kilichopata matokeo ya kura za urais kwa zaidi ya asilimia 10.

“Mimi  nikiwa mgombea urais wa CCM nilipata kura zaidi ya asilimia 91.0, kadhalika hakukuwa na chama cha siasa zaidi ya CCM chenye wingi wa viti vya majimbo katika Baraza la Wawakilishi, kwa hiyo hakuna njia ya mkato kwa mujibu wa katiba kuunda SUK,” alisema.

Aliongeza kuwa kwa msingi huo na kuzingatia kifungu cha 39(3) cha Katiba ya Zanzibar ya 1984, hakuna chama cha siasa kilichokidhi masharti ya kustahiki kutoa Makamu wa Kwanza wa Rais ili kuunda Serikali ya Umoja wa Kitaifa.

“Huo ni uamuzi wa wananchi wa kuipa CCM ushindi mkubwa  na hawakutoa nafasi ya kumchagua Makamu wa Kwanza wa Rais, kwa kuwa walioufanya ni uamuzi wa kidemokrasia,” alisema Dk. Shein.

 Sambamba na hilo alisema uteuzi aliofanya wa kumteua Makamu wa Pili, amefuata masharti ya katiba kifungu 39 (6) kuwa:-

(i) Atateuliwa Makamu wa Pili miongoni mwa wajumbe wa Baraza la Wawakilishi.

(ii) Atoke chama anachotoka Rais. Na kudai uteuzi alioufanya wa kumteua Makamu wa Pili wa Rais umekidhi matakwa ya kifungu 39 (6) cha Katiba ya Zanzibar.

Alisema kwa kifungu hicho kinavyoeleza hakuna njia yoyote ambayo itafanya yeye aunde Serikali ya Umoja wa Kitaifa (SUK) kwa kipindi hiki cha miaka mitano.

 “Nimelazimika kueleza jambo hili la katiba kwa sababu kuna wengine walidhani yupo mgombea anayestahiki kuwa Makamu wa Kwanza wa Rais lakini nimekataa kumteua, kwa kufanya hivyo katiba itakuwa imekiukwa,” alieleza Dk. Shein.

Alisema kitendo chake cha kumteua Balozi Seif Ali Idd kuwa Makamu wa Pili ni sahihi na ni kwa mujibu wa katiba na ameunda serikali kwa kuzingatia muundo wa katiba ya nchi.
Safari za nje, semina ‘stop’

Dk. Shein alisema katika kudhibiti fedha za umma serikali inakusudia kuzuia safari za nje za kikazi zisizo za lazima.
Pia alisema kuwa masuala ya kufanya semina, makongamano na mikutano inayofanywa kwa kutoa posho nono hasa wakati wa kazi yatawekewa utaratibu mpya.

“Manake kuna watu kama hawajaenda nje wanaona hawajafanya kazi, kwa hiyo sasa lazima tuiangalie safari hiyo na umuhimu wake,” alisema Dk. Shein.

Alisema wameamua kubana matumizi kwa kuyaondoa na kutoyafanya mambo ambayo hayana ulazima katika nchi ya Zanzibar.

“Tutafanya tuwezalo ili tuweze kufanikiwa katika hali ya kubana matumizi kwa njia tofauti,” alisema Dk. Shein.

Alisema serikali yake ya Awamu ya Saba inakusudia kuongeza kasi ya ukusanyaji mapato kutoka Sh. Bilioni  362.8 mwaka 2014/2015 hadi  Sh. Bilioni 800 mwaka 2020/2021.
“Ni muhimu kupunguza utegemezi hatua kwa hatua ili baadaye tuweze kujitegemea katika kupanga na kutekeleza mipango yetu ya maendeleo,” alisema Dk. Shein.

Maadili ya Viongozi

Alisema atahakikisha kuwa Tume ya Maadili ya Viongozi wa Umma inafanya kazi ipasavyo ili viongozi wote waliotajwa katika sheria ya maadili ya viongozi wa umma wanatangaza mali zao kwa mujibu wa sheria.

“Kila kiongozi atatakiwa atekeleze hili kwa mujibu wa muda ambao umewekwa,” alieleza Dk. Shein.

Sambamba na hilo katika hali ya kupambana na rushwa na uhujumu uchumi, alisema serikali haitamvumilia mtu yeyote atakayebainika kuzibeza na kutaka kuzirudisha nyuma juhudi za maendeleo kwa udhaifu wa maadili ya kiongozi fulani.

“Hapana asiyejua kuwa rushwa ni adui wa haki na Mwenyezi Mungu ameikataza na kulikemea jambo hilo katika kitabu kitukufu cha Kurani,” alisema Dk. Shein.

Alisema serikali yake inaichukia na inaipiga vita rushwa, ndiyo maana imetengenezwa sheria ya kuzuia rushwa na uhujumu uchumi.

“Wananchi wetu wanaichukia sana na imekuwa bughudha kwao, kwa kuwa hawawezi kupata huduma kama hawajatoa kitu kidogo,” alisema Dk. Shein.

Alisema watawachunguza viongozi wanaofanya vitendo hivyo kwa kuzingatia sheria na taasisi zake ili kujua ukweli na hatimaye kuchukuliwa hatua stahiki.

“Tukiyabaini majipu hayo, tutayatumbua na tutahakikisha hadi moyo umetoka, tunasema sasa basi, tufanyeni kazi,” alisema Dk. Shein.

Dk. Shein aliahidi kuteketeza majipu hayo kwa kila mtu atakayebainika kutenda makosa ya rushwa na uhujumu uchumi na kwenda kinyume cha maadili.

“Nataka kuwahakikishia wananchi kuwa kauli yangu hii si mdomo mtupu, vitendo vitafuata na mtaviona,” alisema Dk. Shein.

Uteuzi

Wakati huohuo, Rais wa Zanzibar na Mwenyekiti wa Baraza la Mapinduzi kwa mujibu ya uwezo aliopewa na Katiba ya Zanzibar kifungu cha 66, amefanya uteuzi wa nafasi 10 za Rais kwa kuwateua wajumbe saba watakaoingia katika Baraza la Wawakilishi.

Miongoni mwa wajumbe walioteuliwa walikuwa ni wagombea watatu wa urais katika uchaguzi uliopita; Hamad Rashid Muhammed (ADC), Juma Ali Khatib (TADEA) na Said Sudi Said (AFP).

Wengine ni aliyekuwa Waziri wa Nchi Ofisi ya Makamu wa Pili wa Rais, Muhammed Aboud Muhammed, Maulin Castico na Balozi Ali Karume.
Wajumbe hao walioteuliwa jana wanategemewa kuapishwa katika kikao kitakachofanyika leo katika Baraza la Wawakilishi Chukwani, Zanzibar. Chanzo Tanzania Daima

No comments:

Post a Comment

Pages