HABARI MSETO (HEADER)


Breaking

December 05, 2025

Mahafali Shivo Education Centre yafana, wazazi, walezi ‘wapigwa msasa’

NA SALUM MKANDEMBA


WAZAZI na walezi nchini wametakiwa kuiunga mkono Serikali kwa kufanya uwekezaji katika elimu ya watoto wao, sambamba na kupiga vita ukatili wa kingono, kijinsia na kuwaepusha na migogoro ya kimahusiano inayowagusa moja kwa moja watoto na kukwaza ustawi wao kitaaluma.




Wito huo umetolewa na Afisa Msaidizi wa Ustawi wa Jamii, Kata ya Ukonga, Danford Moya, wakati wa Sherehe za Mahafali ya 18 ya Shule ya Awali ya Shivo Education Center, iliyopo Mtaa wa Sabasaba, Ukonga Madafu wilayani Ilala jijini Dar es Salaam, zilizofanyika Jumatano Desemba 3, 2025.


Akizungumza na wazazi na walezi wa wanafunzi wa kituo hicho kilichobobea katika Elimu na Malezi ya Watoto, Moya alisema Serikali ya Rais, Dk. Samia Suluhu Hassan imefanya na inaendelea kufanya uwekezaji mkubwa, sambamba na maboresho, yanayopaswa kuungwa mkono na wadau wa sekta hiyo.



 “Moja ya vipaumbele vya Serikali yetu ni pamoja na Sekta ya Elimu, imefanya na inaendelea kufanya mengi makubwa kwa maendeleo na ustawi wa elimu kwa ngazi zote, kuanzia katika Shule za Awali, Msingi, Sekondari, hadi Vyuo vya Kati na Vyuo Vikuu kote nchini.


“Kupitia idara zake, ikiwemo ya Ustawi wa Jamii, wajibu wetu ni kusimamia wadau wa elimu kuhakikisha wanatoa elimu inayokidhi matakwa ya Serikali. Wazazi na walezi, pamoja na wadayu wa elimu nchini, mnapaswa kuiunga mkono Serikali katika hili,” alisema Moya mbele ya waalikwa wa mahafali hayo.



Alifafanua kuwa: “Kwa kuwa leo niko hapa kuzungumza na wazazi, walezi, uongozi na walimu wa Shivo Education Centre, wito wangu kwenu ni kuwa, jitahidini kadri muwezavyo kutimiza wajibu wenu kwa kuhakikisha watoto wanapata haki ya kusoma, bila kukwamishwa na changamoto zozote.”


Aliwataka wazazi hao kuhakikisha wanatimiza wajibu wao huo kwa kuwalinda na kuwaepusha watoto wao na ukatili wa kijinsia na kingono ambao umeshamiri katika jamii, sambamba na kuwaepusha na migogoro ya kimahusiano na kijamii, ili kujenga msingi imara wa elimu akilini na mioyoni mwa watoto.



“Kwa sasa dunia imebadilika, wazazi walindeni na hakikisheni watoto wenu hawaguswi kwa namna yoyote na ukatili wa kingono. Waepusheni na mazingira yanayoruhusu ukatili huo kufanyika, ikiwamo kutowalaza vitandani na wageni tunaowapokea. Msiwaamini sana ndugu, ndio watesi wa watoto wenu hao.


“Hiyo ni pamoja na kuhakikisha migogoro ya kimahusiano mliyonayo wazazi, haiathiri taaluma, ustawi na ukuaji wa mtoto. Kichwa cha mtoto ni kama CD isiyo na kitu, sasa Shivo Education Centre wametimiza wajibu wao kwa kuingiza ‘material’ mazuri vichwani mwa watoto hawa, wajibu wa wazazi ni kuwaendeleza,” alisisitiza Moya.



Aidha, Moya aliwataka wazazi kuhakikisha wao wenyewe na watoto wao, wanajiunga na Mfuko wa Afya wa Jamii (CHF Iliyoboreshwa), ambao ni mpango, muhimu na wa hiari ulioanzishwa na Serikali ya Tanzania kwa wananchi wasio katika mfumo rasmi wa ajira ili kupata bima ya afya nafuu zaidi


“Ili mtoto asome kwa uhuru anapaswa kuwa na CHF Iliyoboreshwa, ambayo mnaweza kujiunga kwa kujiandikisha katika Ofisi za Kata au za Serikali za Mitaa mnapoishi. Hata nyie wazazi, ili maradhi yasiwakwamishe kufanya kazi na kupata pesa za kukidhi mahitaji ya watoto na familia, mnahitaji CHF,” alisema Moya. 

 


Awali, Mkurugenzi na Mwanzilishi wa Shivo Education Centre, Edwin Paulinus Paulo, aliwashukurui wazazi na walezi wa watoto waliohitimu na wale wanaoendelea na masomo shuleni kwake kwa moyo ya kujitoa kuchangia ustawi wa elimu ya vijana wao na kituo kwa ujumla.


Aliwapongeza wazazi na walezi kwa kusaidia maboresho mbalimbali wakati walipohamisha kituo kutoka sehemu moja kwenda nyingine na kwamba thamani ya misaada yao inaakisi dhamira waliyonayo katika kuhakikisha watoto wanajengewa msingi imara wa elimu wakiwa katika shule za awali.



“Wakati tukihamia katika kituo cha sasa, changamoto zilikuwa ni nyingi katika kufanikisha maboresho, lakini wazazi na walezi mlijitoa kutusaidia kuhakikisha watoto wetu wanakuwa kwenye mazingira yanayowapa uhuru wa kujifunza, na katika hili napenda kuwashukuru wote,” alisisitiza Edwin.


Mkurugenzi huyo alitoa wito kwa wazazi, walezi na wadau wa elimu nchini kuendelea kuisapoti Shivo Education Centre, ambayo kwa sasa ina uhitaji wa vifaa vya kukamilisha ujenzi wa Ofisi ya Mkuu wa Shule, Ofisi ya Walimu na Jiko la Kupikia chakula cha watoto shuleni hapo.



Kwa nyakati tofauti wakati wa mahafali hayo, baadhi ya wazazi waliopata fursa ya kuzungumza waliushukuru uongozi wa Shivo Education Centre kwa namna inavyojenga misingi imara ya elimu kwa watoto wao, ushahidi ukiwa ni ufaulu mzuri walionao vijana wao walioko vyuoni, shule za sekondari na za msingi kwa sasa.









No comments:

Post a Comment

Pages