Na Mwandishi Wetu, Dodoma
MKUU wa mkoa wa Dodoma, Jordan Rugimbana ameipongeza
timu ya Uchukuzi SC kwa kuleta wachezaji wengi kwenye mashindano ya Mei Mosi
yaliyoanza Aprili 18 mwaka huu kwenye uwanja wa Jamhuri Dodoma.
Mh. Rugimbana katika hotuba ya ufunguzi wa
mashindano hayo iliyosomwa jana na Afisa Maendeleo Vijana wa ofisi ya mkuu wa
mkoa, Tumsifu Mwasambale kwa niaba yake, alisema kuwa amedokezwa na waandaaji
kuwa Uchukuzi SC ndio timu pekee iliyoweza kuleta wachezaji wengi, hivyo
anawapongeza viongozi wao.
“Ninaipongeza Uchukuzi SC pamoja na kudokezwa pia
nimeona kwa macho yangu wakati wa maandamano ya timu zikiingia uwanjani kuwa Uchukuzi SC ndio wenye wachezaji wengi
zaidi, nawapongeza sana viongozi wao, wanatambua umuhimu wa michezo mahala pa
kazi,” alisema.
Kwa mujibu wa Katibu Mkuu wa timu ya Uchukuzi SC,
Alex Temba amesema timu yake imekuja na wachezaji takribani 96 ambao
watashiriki kwenye michezo ya kuvuta kamba, netiboli, riadha, kuendesha
baiskeli, soka, bao, karata na darts.
Tayari timu hiyo inayoundwa na wachezaji kutoka
Mamlaka ya Viwanja vya Ndege (TAA), Bandari (TPA), Anga (TCAA), Hali ya Hewa
(TMA) na Chuo cha Bandari (DMI), imeshinda
kwenye mechi zake za soka dhidi ya Ukaguzi magoli 3-1 na upande wa netiboli
waliwafunga CDA magoli 23-15.
Hatahivyo, Mh. Rugimbana aliwashutumu na kusema
sababu zilizotolewa na viongozi hao kuzuia timu zao kushiriki kwenye mashindano
ya mwaka huu kwa kisingizio cha Mh. Rais John Magufuli kuzuia michezo hii, hazina
mashiko na ni kisingizio kilichopaswa kukemewa vikali.
Alisema hajawahi
kumsikia Mh. Rais Magufuli akizuia michezo ya Mei Mosi, na mingine
yeyote bali walimsikia akitoa maelekezo ya kuzuia sherehe za Uhuru na sasa
Muungano, na kutoa maelekezo na tayari yanmefatwa kwa ufanisi mkubwa na
wahusika.
“Ni uoga usiokuwa na mashiko, kwani hata ingekuwa Mh
Rais kazuia michezo, hata Mh. Waziri
Mkuu (Kassim Majaliwa) asingekuwa na nguvy ya kukutana na viongozi wa
mashirikisho na vyama vya michezo Uwanja wa Taifa, Dar es Salaam, takribani miezi
mitatu iliyopita wakijadili uimarishaji wa michezo, na walaumu sana
viongozi waliowanyima haki wanamichezo
kushiriki kwenye michezo hii,” alisema Rugimbana.
Mashindano ya mwaka huu yenye kauli mbiu ya hapa kazi tu isiwe kisingizio kwa waajiri
kuondoa michezo kazini, yamekuwa na idadi ndogo ya washiriki, ambapo hadi
jana ni timu 14 pekee ndizo zilizofika Dodoma.
Hatahivyo, awali Kaimu Makamu Mwenyekiti wa Kamati
ya Mei Mosi, Joyce Benjamin, naye katika hotuba ya ufunguzi aliwalaumu viongozi
kuzuia timu zao kwa kumsingizia Mh. Rais kuwa amezuia michezo.
“Kumbukeni
Mh. Rais wetu ni mmoja wa wanamichezo na ndio maana hata wakati wa kampeni
tulimuona wote akipiga pushapu jukwaani, sasa iweje leo hii viongozi wa sehemu
za kazi waseme amekataza michezo, michezo huu ni mikubwa imepata Baraka zote
kutoka TUCTA (Shirikisho la Vyama vya Wafanyakazi) na Baraza la Michezo la
Taifa (BMT),” alisema Benjamin.
Bendi ya Watoto
wa shule ya msingi ya St. Tom wakiongoza maandamano ya timu shiriki za
mashindano ya Mei Mosi kuingia uwanjani.
Kaimu Makamu Mwenyekiti wa Kamati ya Mashindano ya Mei Mosi, Joyce Benjamin akitoa hutoba yake.
Mgeni rasmi Afisa Maendeleo Vijana,, Tumsifu Mwasambale akitoa hotuba alipiomwakilisha mkuu wa mkoa wa Dodoma, Mh. Jordan Rugimbana.
Timu ya Uchukuzi SC wakiwa wamejipanga uwanjani wakimsikiliza mgeni rasmi, Afisa Maendeleo Vijana, Tumsifu Mwasambale (hayupo pichani).
No comments:
Post a Comment