Na Mwandishi Wetu, Dodoma
MWENDESHA baiskeli Chaptele Muhumba wa Uchukuzi SC, jana
alitwaa ubingwa wa saba wa mashindano ya Mei Mosi ya kilometa 35 kwa wanaume yaliyoendelea
kwenye uwanja wa Jamhuri mkoani hapa.
Chaptele, ambaye hana mpinzani alianza kutwaa
ubingwa katika mashindano yake ya kwanza mwaka 2010 yaliyofanyika Morogoro
kitaifa, na baadaye kufululiza kutwa ubingwa ikiwa ni mara mbili zaidi mkoani
Morogoro, na mara moja-moja kwenye mikoa ya Mbeya, Tanga na Mwanza.
Lakini, mchezaji huyo aliyemaliza kwa kutumia muda
wa 1:27:42 aliwataka waandaaji kuhakikisha wanaongeza askari wa usalama wa
barabarani, ili kuzuia madereva wakorofi wanaoingilia msafara wao, ambapo
unahatarisha usalama wao.
“Askari wa usalama wawili tu hawatoshi, kama
mlivyoona magari makubwa malori yanatupita na mara ghafla yalikuwa yakirudi
upande wetu na wengi tuliingia uoga,” alisema Chaptele.
Katibu Mkuu wa Kamati ya mashindano hayo, Award
Safari alisema suala lililolalmikiwa na wachezaji wa baiskeli ataliwasilisha kwenye
kikao cha viongozi wote wa timu, ambacho hufanyika mara baada ya kumalizika kwa
michezo ya siku husika.
Chaptele alifuatiwa na Peter Ngalu wa TPDC aliyetumia
muda wa 1:30:43 na Irimin Tarimo wa Tanesco alishika nafasi ya tatu kwa 1:40:51,
wakati kwa wanawake bingwa ni Naomi Kimaro wa TPDC katumia muda wa 57:03, huku
mshindi wa pili ni Bertha Wilson wa Ujenzi katumia 58:19 na Salome Luvanda wa
Tamisemi akiwa wa tatu kwa muda wa 59:26.
Katika soka timu
ya Uchukuzi SC ilipata ushindi wa chee baada ya Mambo ya Ndani kushindwa
kutokea uwanjani. Uchukuzi ndio inaongoza kwenye kundi B kwa kuwa na pointi
saba, ikifuatiwa na GGM wenye pointi nne.
Nao TPDC waliwashinda UDOM kwa magoli 2-1. Magoli
yote ya washindi yalifungwa na mshambuliaji Daruwesh Shija katika dakika ya 13
na 54, na bao pekee la UDOM lilipachikwa na Ally Lutavi katika dakika 23.
Kwa upande wa kamba kwa wanawame na wanaume Uchukuzi
SC waliweza kuibuka washindi, ambapo wanawake waliwavuta bila huruma Ukaguzi
kwa mivuto 2-0, na wanaume waliwachapa Tamisemi kwa mivuto 2-0.
Katika mchezo wa draft wanaume Ally Salehe wa
Uchukuzi SC aliibuka mshindi wa pili, baada ya Salum Simba wa Tamisemi kuwa
bingwa na Haji Chillo wa UDOM kushika nafasi ya tatu.
Kwa upande wa draft wanawake mchezaji Stella
Limbumba wa Tanesco alitwaa ubingwa, akifuatiwa na Joyce Kimondi wa Ujenzi na
Chausiku Hamisi wa CDA akiwa wa tatu.
Michuano hii inaendelea leo kwa upande wa soka timu
ya GGM kuumana na Ukaguzi, huku UDOM wakikutana na Tamisemi, nao CDA
wakiwakaribisha Mambo ya Ndani; wakati katika netiboli Tanesco itacheza na CDA .
Thea
Samjela wa Uchukuzi SC (kuilia) akichuana na Regina Mutimangi wa TPDC katika
mchezo wa bao.
Omar Said wa Uchukuzi SC (kushoto) akicheza bao dhidi Hamisi Rahis wa Tanesco.
Ally Sule wa Uchukuzi SC(kushoto) akicheza mchezo wa fainali dhidi ya Salum Simba wa Tamisemi. Simba aliibuka bingwa.
Timu ya wanawake ya kamba ya Uchukuzi SC wakiwavuta wenzao wa Ukaguzi kwa mivuto 2-0.
Timu ya wanaume ya Uchukuzi SC wakiwavuta wenzao wa Tamisemi kwa mivuto 2-0.
Bingwa
wa baiskeli kwa wanawake Naomi Kimaro wa TPDC akimaliza mbio za kilometa 20
zilizoanzia Chigongo na kumalizikia makaburi ya Nkuhungu
Chaptele
Muhuimba wa Uchukuzi SC akimaliza mbio za baiskeli za kilometa 35 kwa kutumia
muda wa 1:27:42.
No comments:
Post a Comment