April 23, 2016

Rais Magufuli hajakataza michezo – Mh. Rugimbana

Na Mwandishi Wetu, Dodoma

MKUU wa mkoa wa Dodoma, Jordan Rugimbana amesema hajawahi  kumsikia Mh. Rais John Magufuli kuzuia michezo ya Mei Mosi, ambayo ilianza Aprili 18 mwaka huu kwenye viwanja vya Jamhuri mkoani Dodoma.

Katika hotuba yake ya uzinduzi wa michezo hiyo iliyosomwa juzi na Afisa Maendeleo Vijana, Tumsifu Mwasambale kwa niaba yake, alisema ameshangazwa na idadi ndogo ya timu shiriki, huku nyingi zikitoa kisingizio kuwa Mh. Rais amekataza michezo hii, ambayo kauli mbiu yake ni ‘Hapa kazi tu isiwe kisingizio kwa waajiri kuondoa michezo kazini’.

“Nashangaa sana kwani nimesikia kuwa timu nyingi, ambazo zilikuwa ndio washiriki wakubwa hazijashiriki kwenye mashindano ya mwaka huu, kwa viongozi wao kusingizia kuwa Mh. Rais amekataza, mimi sijasikia kuhusu hilo kabisa,” alisema.

Alisema kuwa endapo Mh. Rais Magufuli angekuwa amekataza michezo, asingemteuliwa Mh. Nape Nnauye kuwa Waziri wa Wizara ya Habari, Vijana, Sanaa na Michezo, hivyo kuwataka viongozi mahala pa kazi kuacha visingizio vya kumsingizia Rais wakati hajatoa tamko kuhusu hilo.

“Nasema huo ni uoga usiokuwa na mashiko, kwani hata ingekuwa hivyo hata Mh. Waziri Mkuu (Kassim Majaliwa) asingekutana na viongozi wa mashirikisho na vyama vya michezo kule uwanja wa Taifa, Dar es Salaam, miezi mitatu iliyopita kuzungumzia uimarishaji wa michezo, hivyo nawalaumu sana viongozi  waliowanyima haki wafanyakazi wanamichezo kuja kushiriki kwenye michezo hii,” alisema Rugimbana.

Hatahivyo, alisema Mh. Rais Magufuli anachotaka ni uhalisia wa yale yanayofanywa na viongozi wa serikali ni uhakika na kweli na kusiwe na udanganyifu wowote. 

Rugimbana alisema michezo mahala pa kazi inasaidia kujenga na kuimarisha afya za wafanyakazi ili waendelee kutoa huduma bora iliyotukuka kwa wananchi na kuongeza tija zaidi mahala pa kazi, pia husaidia kujenga mahusiano mema ikiwa ni pamoja na kubadilishana mawazo.
Pia aliwataka wachezaji kucheza kwa nidhamu na waache vitendo vya utovu wa nidhamu, kwani hatasita kuripoti kwa waajiri wao.

Awali Kaimu Makamu Mwenyekiti wa Kamati ya Mei Mosi, Joyce Benjamin, naye katika hotuba ya ufunguzi aliwalaani viongozi wa mahala pa kazi kumsingizia Mh. Rais kuwa amezuia michezo na kusababisha mashindano ya mwaka huu kutokuwa na timu nyingi kama miaka ya nyuma.
Benjamin alisema kuwa hadi juzi ni timu 14 pekee zilizofika mkoani hapa kushiriki kwenye mashindano haya, wakati nyingine zikizuiwa na viongozi wao, bila kuwa na sababu za msingi.

“Kumbukeni Mh. Rais ni mmoja wa wanamichezo na ndio maana hata wakati wa kampeni tulimuona wote akipiga pushapu jukwaani, sasa iweje leo hii viongozi wa sehemu za kazi waseme amekataza michezo, michezo huu ni mikubwa imepata Baraka zote kutoka TUCTA (Shirikisho la Vyama vya Wafanyakazi) na Baraza la Michezo la Taifa (BMT),” alisema Benjamin.

Michuano hii inashirikisha michezo ya soka, netiboli, kuvuta kamba, karata, bao, darts, riadha na mbio za baiskeli.

No comments:

Post a Comment

Pages