Na Mwandishi Wetu, Dodoma
TIMU ya soka ya Tanesco imeendeleza wimbi la ushindi
kwa kuwachapa Chuo Kikuu cha Dodoma (UDOM) kwa magoli 3-1 katika mchezo
uliofanyika jana asubuhi kwenye uwanja wa Jamhuri mkoani hapa.
UDOM ndio walikuwa wa kwanza kupata bao katika
dakika ya kwanza ya mchezo lililofungwa na Ally Lutavi, na dakika moja baadaye
Tanesco walisawazisha kwa njia ya penati kupitia Said Kondo baada ya mchezaji
wao kuangushwa katika eneo la hatari.
Mchezaji Khalifa Shekuwe aliiongezea Tanesco bao la
pili katika dakika ya 35 na Joseph Mzee alipigilia msumari wa mwisho kwa
kuandika bao la tatu katika dakika ya 81, ambapo sasa Tanesco wamefikisha
pointi saba.
Katika mchezo mwingine uliochezwa pia kwenye uwanja
huo, timu ya Geita Gold Mine (GGM) waliwafunga CDA Dodoma ‘Watoto wa nyumbani’
kwa magoli 2-0.
Mabao ya GGM yalifungwa na Gwetu Guvete dakika ya 11
na Oscar Binamungu katika dakika ya 13.
Kwa upande wa
mchezo wa netiboli, timu ya Tamisemi inayoundwa na wachezaji wakongwe na
wenye uzoefu waliifundisha TPDC kwa kuwafunga
magoli 40-6. Hadi mapumziko Tamisemi waklikuwa mbele kwa magoli 18-5.
Katika mchezo wa kuvuta kamba wanaume, TPDC
waliwafuta machozi dada zao wa netiboli baada ya kuwavuta bila huruma Tanesco
kwa 2-0.
Michuzno hiyo iliendelea baadaye jioni (jana) kwa
mechi za mchezo wa netiboli za Uchukuzi SC kucheza na Tanesco, huku TPDC
wakiwakaribisha CDA Dodoma, wakati kwa upande wa soka Uchukuzi SC watacheza na
GGM, ambao walichelewa kufika na sasa wanacheza mfululizo.
No comments:
Post a Comment