May 12, 2016

MGODI WA DHAHABU WA BULHANHLU WAINGIA MAKUBALIANO NA TAASISI YA BENJAMINI WILLIAM MKAPA

Meneja Mkuu wa Mgodi wa Bulyanhulu Graham Crew akibadilishana hati za makubaliano na Afisa Mkuu wa Taasisi ya Benjamin William Mkapa,Dkt Ellen Mkondya wakati wa hafla ya makabidhiano ya hati hizo iliyofanyika wilayani Kahama.
Meneja Mkuu wa Mgodi wa Bulyanhulu,Graham Crew pamoja na Afisa Mkuu wa Taasisi ya Benjamin William Mkapa Dkt Ellen Mkondya wakitia saini katika hati za makubaliano ya kuboresha mradi wa huduma ya afya ,Zoezi la utiaji saini ulishuhudiwa na Mkuu wa wilaya ya Kahama ,Vita Kawawa(kulia) ,Mkurugenzi wa Halmashauri ya Msalala,Patrick Karangwa (nyuma ya mkuu wa wilaya) pamoja na viongozi wa Mgodi wa Bulyanhulu ,Elias Kasitila na Mganga Mkuu wa wilaya ya Msalala Dkt Hamad Nyembea.
Meneja wa Mgodi wa Bulyanhulu ,Graham Crew akizungumza mara baada ya kutiliana saini makubaliano ya kuboresha huduma za Afya na Taasisi ya Benjamini William Mkapa wakati wa hafla iliyofanyika katika mji wa Kahama.
Mkuu wa wilaya ya Kahama ,Vita Kawawa akitoa neno la shukrani kwa uongozi wa Mgodi wa dhahabu wa Bulyanhulu kwa michango ambao wameendelea kutoa kwa wilaya ya Kahama na Msalala.

Na Dixon Busagaga wa Globu ya Jamii aliyeko Shinyanga.

MGODI wa dhahabu wa Bulyanhulu ulioko wilayani Kahama umetiliana saini hatii ya makubaliano ya Dola 200,000 sawa na shilingi Milioni 440 za Tanzania na Taasisi ya Benjamin William Mkapa (BMF) kwa ajili ya mradi wa kuboresha huduma za afya ya uzazi kwa mama na mtoto katika wilaya ya Msalala mkoani Shinyanga

Mgodi  Bulyanhulu kupitia Mfuko wa Maendeleo wa Acacia na Taasisi ya Benjamin W. Mkapa (BMF) wamesaini hati ya makubaliano ili kushirikiana katika kutekeleza mradi wa miaka miwili unaolenga kuboresha huduma ya afya ya mama na mtoto katika jamii .

Mgodi wa Bulyanhulu kupitia Mfuko wa Maendeleo wa Acacia utatoa kiasi cha dola za Kimarekani 200,000 kusaidia awamu ya pili ya mradi wa BMF utakaosaidia kuboresha huduma ya vituo viwili vya afya wilayani humo, Kituo cha Afya cha Bugarama na Zahanati ya Kakola kupitia mradi huo.

Mradi huo katika vituo tajwa unatarajiwa kunufaisha wananchi 321,852 katika Halmashauri ya Msalala ambapo makubaliano hayo ya miaka miwili yanaanzia, 01 April 2016 hadi 30 Machi 2018.

“Mgodi wetu unaendesha shughuli zake katika halmashauri ya Msalala hapa mkoani Shinyanga na sehemu ya uwajibikaji wetu kwenye jamii, kupitia mkakati wa mipango endelevu kwenye jamii na kusaidia mikakati ya uboreshaji wa sekta ya afya kwa ajili ya jamii inayozunguka mgodi.”alisema Graham Crew.

“Ushirikiano huu na Taasisi ya BMF umekuja wakati muafaka ambapo BGML imewekeza katika miundombinu ya kuipandisha hadhi zahanati ya Bugarama kuwa kituo cha afya na pia kumalizia ujenzi wa Zahanati ya Kakola.” Aliongeza meneja huyo mkuu wa Mgodi wa Dhahabu wa Bulyanhulu Graham Crew.

Awamu ya pili ya Mradi wa BMF inalenga kutekeleza mradi utakaoboresha huduma za HIV/AIDS, huduma za mama na mtoto kwa kuongeza upatikanaji wa wataalamu wa afya na kuboresha miundombinu ya kutolea huduma za afya.

Afisa Mtendaji Mkuu wa BMF Dk Ellen Mkondya Senkoro amesema; “Takwimu zinaonyesha kwamba mkoa wa Shinyanga una maambukizi kwa asilimia 7.4% ambapo kiwango kikubwa kipo katika halmashauri ya Msalala kutokana na shughuli za uchimbaji madini hasa uchimbaji mdogo mdogo.”

“Kiwango hiki kimeendelea kuwa hivyo tangu mwaka 2007/2008 hadi 2011/2012 ingawa kiwango cha maambukizi nchini kimepungua kutoka asilimia 5.7% hadi 5.1% hivyo sehemu hii inahitaji hatua maalumu. “alisema Dkt Mkondya.

Alishukuru Kampuni ya  ACACIA kwa msaada huo na kwamba utasaidia kwenye utekelezaji wa uboreshaji wa mifumo ya kukabiliana na tatizo la Virusi vya Ukimwi, huduma za uzazi na watoto kwa kuongeza rasilimali watu ya watalaamu wa afya, uendelezaji wa miundombinu na kujengea uwezo maeneo yanayohitaji ufanisi zaidi.

 Tangu mwaka 2013 Taasisi ya Benjamin William Mkapa (BMF) imekuwa ikishirikiana na Acacia kupitia Mfuko wake wa Acacia Maendeleo Fund katika kutekeleza sehemu ya miradi ya awamu ya pili ya mfuko wa taasisi ya BMF katika wilaya ya Biharamulo mkoani Kagera na Halmashauri iliyokuwa ya Kahama mkoani Shinyanga.

Kuhusu Mfuko wa Maendeleo wa Acacia:
Mfuko wa Maendeleo wa Acacia maarufu kama Acacia Maendeleo Fund ulianzishwa mwaka 2011 kama sehemu ya dhamira katika kuboresha maendeleo endelevu katika jamii kwenye maeneo tunayofanya kazi. Hadi sasa tumefanikiwa kuwekeza dola za kimarekani milioni 35.0 katika miradi 150 kwenye maeneo mbalimbali.

Misaada kutoka kwenye mfuko huu hutoa kipaumbele kwa vitega uchumi vinavyosaidia maendeleo ya jamii, ujengaji wa uwezo, sekta ya afya, elimu, maji, mazingira katika maeneo tunakoendesha shughuli zetu.

Taasisi ya Benjamin W. Mkapa 
Taasisi ya Benjamin W. Mkapa ilianzishwa April 2006 na Rais Mtaafu wa Jamuhuri ya Muungano wa Tanzania Mheshimiwa Benjamin W. Mkapa, taasisi hii isiyo ya kiserikali ina dhamira ya kuboresha afya na hali za watanzania hasa katika maeneo yaliyoko vijijini kwa kutekeleza miradi yenye kutoa matokeo.

No comments:

Post a Comment

Pages