WAZIRI MKUU Kassim Majaliwa amesema Jumuiya ya Madola inaweza kuiga mbinu ambazo Tanzania imetumia katika kupambana na rushwa zikiwemo za kujumuisha wadau tofauti kwenye vita hiyo.
Ametoa kauli hiyo mwishoni mwa wiki wakati akizungumza na Katibu Mkuu wa Jumuiya ya Madola, Bibi Patricia Scotland walipokutana kwenye mkutano wa kimataifa uliojadili jinsi ya kupambana na rushwa duniani uliofanyika Lancaster House, jijini London, Uingereza.
“Tanzania iko tayari kushirikiana na ninyi katika kujenga timu hii na ili uweze kupata picha halisi, nakukaribisha Tanzania uje ujionee hatua ambazo tumechukua hadi kufikia hapa tulipo kwenye vita hii dhidi ya rushwa,” alisema Waziri Mkuu ambaye alihudhuria mkutano huo kwa niaba ya Rais Dk. John Pombe Magufuli.
Alimweleza Katibu Mkuu huyo kwamba Serikali ya Awamu ya Tano imefanikiwa kupambana na rushwa kutokana na ushirikiano mkubwa inaoupata kutoka kwa wananchi. “Wananchi wanafurahia juhudi za Serikali, vyama vya kiraia pia vinaunga mkono jitihada zetu na vyombo vya habari vinashirikiana nasi katika vita hii,” alisema.
Waziri Mkuu alitoa wito huo baada ya kuelezwa na Bibi Scotland kwamba anataka kuanzisha idara malum kwenye Jumuiya hiyo ambayo itasimamia mapambano dhidi ya rushwa na makosa ya jinai.
“Nataka tuwe na idara yenye watu mahiri wa idara za uhasibu, mahakama yenyewe ikiwemo waendesha mashtaka na wanasheria kutoka kwenye nchi kadhaa ili washirikishane uzoefu kutoka kwenye nchi zao. Ninaamini katika nchi 53 ambazo ni wanachama wetu, sitakosa watu wa aina hii,” alisema.
Alisema ameamua kufanya hivyo ili aweze kuendanana na malengo makuu matatu ya jumuiya hiyo ambayo ni kupiga vita rushwa, kuhimiza utawala bora na usimamizi wa demokrasia.
IMETOLEWA NA:
OFISI YA WAZIRI MKUU
JUMAMOSI, MEI 14, 2016.
No comments:
Post a Comment