May 26, 2016

Zawadi Azania Bank Kids Run zatajwa

 Mjumbe wa Kamati ya Utendaji ya shirikisho la Riadhaa Tanzania (RT), Tullo Chambo akizungumza wakati wa mkutano na waandishi wa habari jijini Dar es Salaam leo, kuhusu mbio maalum za watoto zijulikanazo Azania Bank Kids Run zitakazofanyika juni 5 katika viwanja vya Mnazi Mmoja jijini. Kushoto ni Ofisa Masoko Mwandamizi wa Azania Bank, Othman Jibrea na kulia ni mratibu wa mbio hizo, Wilhelm Gidabuday. (Na Mpiga Picha Wetu)
Ofisa Masoko Mwandamizi wa Azania Bank, Othman Jibrea, akizungumza wakati wa mkutano na waandishi wa habari jijini Dar es Salaam leo kuhusu mbio maalum za watoto zijulikanazo Azania Bank Kids Run zitakazofanyika juni 5 katika viwanja vya Mnazi Mmoja jijini. Kulia ni Mjumbe wa Kamati ya Utendaji ya shirikisho la Riadhaa Tanzania (RT), Tullo Chambo.

Na Mwandishi Wetu

WADHAMINI wakuu wa Mbio za Watoto za Azania Bank Kids Run 2016, Benki ya Azania, wametangaza zawadi za washindi wa mbio hizo zitakazofanyika viwanja vya Mnazi Mmoja, jijini Dar es Salaam, Juni 5.

Akizungumza na waandishi wa habari kwenye Ukumbi wa Mikutano wa Baraza la Michezo la Taifa (BMT), Ofisa Masoko Mwandamizi wa Azania Bank, Othman Jibrea, alisema benki yake inajisikia fahari kuwekeza katika mbio hizo za watoto.

Alizitaja zawadi za mbio za kilomita 5 kuwa ni Sh. 200,000 kwa mshindi wa kwanza, Sh. 150,000 kwa mshindi wa pili na Sh. 100,000 kwa mshindi wa tatu, wote wakitarajiwa pia kupata medali, begi lenye vifaa vya shule na vya michezo.

Jibrea alibainisha kuwa mshindi wa kwanza wa mbio za Kilomita 2 atajinyakulia Sh. 100,000, mshindi wa pili Sh. 75,000 na mshindi wa tatu Sh. 50,000, pamoja na medali, begi lenye vifaa vya shule na sare za michezo.

Katika mbio za Kilomita 1, Jibrea alitaja zawadi za washindi kuwa ni Sh. 75,000 kwa mshindi wa kwanza, Sh. 50,000 kwa mshindi wa pili na Sh. 40,000 kwa mshindi wa tatu, ambao watapata zawadi ya ziada ya medali, begi lenye vifaa vya shule na michezo.

“Pia washindi wa nne hadi wa 10 wa mbio hizo, watapata kifuta jasho cha Sh. 15,000, begi lenye vifaa vya shule na michezo. Nia ni kuwafanya watoto watakaoshiriki kutotoka bure mwishoni mwa mashindano, na zawadi zote za fedha taslimu tutawawekea kwenye akaunti tutakazowafungulia katika Benki ya Azania,” alisema Jibrea.

Ofisa huyo alifichua kilichowasukuma Azania Bank kudhamini mbio hizo kuwa ni kurejesha sehemu ya pato lake kwa jamii, lakini pia kuwa sehemu ya kuiwezesha jamii kujenga kizazi imara kinachoshiriki michezo kwa ustawi wa taifa.

Kwa upande wake Mratibu wa Azania Bank Kids Run 2016, Wilhelm Gidabuday, aliishukuru Azania Bank kwa kukubali kusapoti mbio hizo, na kuongeza kwamba kwa kuwa msingi wa michezo yote ni mbio, basi anaamini Azania imewekeza mahali sahihi.

“Hakuna mchezo duniani usiohusisha mazoezi ya kukimbia ama usiohitaji mshiriki kuwa na mbio, iwe soka, ngumi, tenisi, nk. Ndiyo kusema Azania imefanya uamuzi sahihi na tunawaomba wazazi na walezi wawasajili watoto wao kwa ada ya Sh. 2,000,” alisema.

Alibainisha kuwa fomu za ushiriki zinapatikana katika matawi ya Azania Bank popote jijini Dar es Salaam, ofisi za Shirikisho la Riadha Tanzania (RT), pamoja na Ofisi za BMT zilizoko Samora Avenue katikati ya jiji.

No comments:

Post a Comment

Pages