July 18, 2016

WANAWAKE WAFUGA NYUKI KUOKOA MISITU YA PUGU NA KAZIMZUMBWI

Maofisa wa taasisi ya Mfuko wa Wanawake wa Afrika (WAF) Anna Salado na Alicia (kushoto) wakipata maelezo ya fugaji nyuki katika msitu wa hifadhi wa Pugu.

WANAWAKE wanaofuga nyuki wataokoa hekta 7,270 za misitu ya hifadhi ya Pugu na Kazimzumbwi, imefahamika.
Misitu hiyo, ambayo ni miongoni mwa Misitu ya Hifadhi 486 iliyopo nchini, imekuwa hatarini kutoweka kutokana na shughuli za kijamii hususan uvamizi wa mipaka na ukataji wa miti kwa ajili ya uchomaji mkaa ambao kwa muda mrefu umekuwa ukifanywa na wananchi mbalimbali.

Meneja wa Misitu hiyo kutoka Wakala wa Huduma za Misitu (TFS), Mathew Mwanuo, anasema kwamba, misitu hiyo iliyopo katika wilaya za Ilala mkoani Dar es Salaam na Kisarawe mkoani Pwani, imekuwa hatarini kutoweka licha ya jitihada za serikali za kukabiliana na wavamizi hao.

“Lakini sasa miradi hii ya ufugaji nyuki inayowahusisha wanawake wa Pugu na Kisarawe itakuwa mkombozi kwa sababu wananchi wenyewe wanahusishwa moja kwa moja na suala la ulinzi,” anasema Mwanuo wakati akiwaelekeza wageni kutoka taasisi ya Mfuko wa Wanawake wa Afrika (WAF) kutoka nchini Hispania waliotembelea miradi hiyo hivi karibuni.

Mwanuo anasema kwamba, ndani ya misitu hiyo ya hifadhi kuna jumla ya vikundi vinne vya akinamama vinavyojihusisha na ufugaji wa nyuki wa kisasa, ambapo viwili vinafadhiliwa na mradi wa Green Voices Tanzania na viwili vinafadhiliwa na TFS.
Anna Salado akiwa msituni kuangalia ufugaji wa nyuki kwenye hifadhi ya Pugu.

“Kazi ni kubwa katika kuilinda misitu hii, tunao askari wetu wanaozunguka humu, lakini hawatoshi kuweza kuzunguka maeneo yote na ndiyo maana huko nyuma watu walikuwa wakivamia kukata miti na kuchoma mkaa.

“Zamani ulikuwa ukipita pembeni unaona misitu inapendeza, lakini ukiingia ndani kulikuwa na watu wanachoma mkaa huku mambo mengine yakiendelea kama uuzwaji wa vinywaji na kadhalika… yaani hali ilikuwa mbaya sana,” anasema.

Mshiriki kiongozi wa miradi hiyo ya ufugaji wa nyuki chini ya Green Voices, Monica Kagya, anasema kwamba, anaishukuru taasisi ya Mfuko wa Wanawake Afrika (WAF) kwa kumwezesha yeye na wenzake 14 kupata mafunzo nchini Hispania mapema mwaka huu ili kuwapa uwezo wanawake kushiriki shughuli za utunzaji wa mazingira na kukabiliana na mabadiliko ya tabianchi.

No comments:

Post a Comment

Pages