Maofisa
wa taasisi ya Mfuko wa Wanawake wa Afrika (WAF) Anna Salado na Alicia
(kushoto) wakipata maelezo ya fugaji nyuki katika msitu wa hifadhi wa
Pugu.
WANAWAKE
wanaofuga nyuki wataokoa hekta 7,270 za misitu ya hifadhi ya Pugu na
Kazimzumbwi, imefahamika.
Misitu hiyo,
ambayo ni miongoni mwa Misitu ya Hifadhi 486 iliyopo nchini, imekuwa hatarini
kutoweka kutokana na shughuli za kijamii hususan uvamizi wa mipaka na ukataji
wa miti kwa ajili ya uchomaji mkaa ambao kwa muda mrefu umekuwa ukifanywa na
wananchi mbalimbali.
Meneja wa
Misitu hiyo kutoka Wakala wa Huduma za Misitu (TFS), Mathew Mwanuo, anasema
kwamba, misitu hiyo iliyopo katika wilaya za Ilala mkoani Dar es Salaam na
Kisarawe mkoani Pwani, imekuwa hatarini kutoweka licha ya jitihada za serikali
za kukabiliana na wavamizi hao.
“Lakini sasa
miradi hii ya ufugaji nyuki inayowahusisha wanawake wa Pugu na Kisarawe itakuwa
mkombozi kwa sababu wananchi wenyewe wanahusishwa moja kwa moja na suala la
ulinzi,” anasema Mwanuo wakati akiwaelekeza wageni kutoka taasisi ya Mfuko wa
Wanawake wa Afrika (WAF) kutoka nchini Hispania waliotembelea miradi hiyo hivi
karibuni.
Mwanuo anasema
kwamba, ndani ya misitu hiyo ya hifadhi kuna jumla ya vikundi vinne vya
akinamama vinavyojihusisha na ufugaji wa nyuki wa kisasa, ambapo viwili
vinafadhiliwa na mradi wa Green Voices Tanzania na viwili vinafadhiliwa na TFS.
Anna Salado akiwa msituni kuangalia ufugaji wa nyuki kwenye hifadhi ya Pugu.
“Kazi ni
kubwa katika kuilinda misitu hii, tunao askari wetu wanaozunguka humu, lakini
hawatoshi kuweza kuzunguka maeneo yote na ndiyo maana huko nyuma watu walikuwa
wakivamia kukata miti na kuchoma mkaa.
“Zamani
ulikuwa ukipita pembeni unaona misitu inapendeza, lakini ukiingia ndani
kulikuwa na watu wanachoma mkaa huku mambo mengine yakiendelea kama uuzwaji wa
vinywaji na kadhalika… yaani hali ilikuwa mbaya sana,” anasema.
Mshiriki kiongozi
wa miradi hiyo ya ufugaji wa nyuki chini ya Green Voices, Monica Kagya, anasema
kwamba, anaishukuru taasisi ya Mfuko wa Wanawake Afrika (WAF) kwa kumwezesha
yeye na wenzake 14 kupata mafunzo nchini Hispania mapema mwaka huu ili kuwapa
uwezo wanawake kushiriki shughuli za utunzaji wa mazingira na kukabiliana na mabadiliko
ya tabianchi.




No comments:
Post a Comment