WAZIRI MKUU Kassim Majaliwa amepokea michango yenye thamani ya sh. milioni 660.25 zikiwa ni fedha taslimu, hundi na vifaa mbalimbali kwa ajili ya wananchi walioathirika na tetemeko la ardhi lililotokea mkoani Kagera, mwezi uliopita.
Makabidhiano ya michango hiyo, yamefanyika leo mchana (Jumanne, Oktoba 11, 2016) kwenye ukumbi wa Ofisi ya Waziri Mkuu, Magogoni jijini Dar es Salaam.
Akikabidhi hundi ya mfano kwa Waziri Mkuu, Makamu wa Rais wa kampuni ya ACACIA, Bw. Deodatus Mwanyika amesema wao wametoa sh. milioni 325 ambazo tayari wameshaziingiza kwenye akaunti ya maafa.
Amewaomba wadau wengine na taasisi nyingine hapa nchini wajitokeze kuisaidia Serikali kukabiliana na janga hili kwani mahitaji halisi ni makubwa kuliko kiasi ambacho kimekusanywa hadi sasa.
Wadau wengine waliochangia ni Balozi wa Japan nchini, Bw. Masaharu Yoshinda pamoja na Shirika la Misaada la Maendeleo la Japan (JICA) ambao wametoa vifaa vyenye thamani ya sh. milioni 220. Vifaa hivyo ni mahema 220, mablanketi 1,100; vigodoro vyepesi (sleeping pads) 1,110; madumu ya maji 250 na plastic sheets 22.
Naye Mkurugenzi Mkuu wa TBC1, Dk. Ayoub Rioba ambaye alikabidhi hundi za sh. milioni 41.55, amesema kama taasisi waliguswa na tatizo la maafa ya Kagera kwa hiyo wakatafuta njia ya kuchangisha ili wapate fedha za kuisaidia Serikali kukabiliana na tatizo hilo.
“Tuliamua kufanya harambee na kuwahamasisha wananchi wachangie ambapo wengine walileta kwetu na wengine wakapeleka moja kwa moja Kagera. Na leo tunakabidhi kiasi ambacho tulikikusanya kupitia harambee hiyo,” amesema.
Wengine waliokabidhi michango yao, ni Makamu Mwenyekiti wa Umoja wa Wenye Magereji Tegeta, Bw. Leonard Mwanjela ambaye ametoa fedha taslimu sh. milioni mbili kwa niaba ya mafundi gereji wilaya ya Kinondoni. Naye Katibu Mkuu wa Jumuiya ya Wafanyabiashara Kariakoo (JWK), Bw. Abdalla Mwinyi amesema walifanya harambee na kupata sh. milioni 60.8 ambazo wameamua kununua nguo na magodoro, unga wa mahindi tani 10.
Wengine ni Taasisi ya Wakaguzi wa Ndani (Internal Audit) ambao wamekabidhi sh. milioni 6.7. Mwenyekiti wa Bodi wa taasisi hiyo, Bw. Richard Magongo amesema baada ya kuona hilo, waliamua kuchangishana na kupata kiasi hicho cha fedha.
Naye Mkurugenzi wa Kampuni ya Sura Technologies, Bw. Ramadhar Reddy amekabidhi hundi ya sh. milioni 5 kwa ajili ya kuwasaidia wananchi waliokumbwa na maafa hayo.
Akitoa shukrani kwa waliotoa michango hiyo, Waziri Mkuu amewashukuru wote kwa misaada yao na kuahidi kuwa Serikali itahakikisha michango hiyo inafikishwa Kagera kwa walengwa.
“Tunawashukuru sana kwa michango yote. Kutoa ni moyo na siyo utajiri. Nawaomba Watanzania wengine muendelee kujitokeza ili tuweze kuwasaidia wenzetu waliokumbwa na maafa haya,” amesema.
Pia amewashukuru waandishi wa habari kwa kuwapa wananchi taarifa za matukio hayo na kuwahamasisha wachangie ndugu zao waliokumbwa na maafa ya tetemeko la ardhi. Tetemeko hilo lilitokea, Septemba 10, mwaka huu na kusababisha vifo vya watu 17 na wengine 440 kujeruhiwa.
Pia tetemeko hilo limesababisha nyumba 2,063 kuanguka huku nyingine 14,081 zikiwa katika hali hatarishi baada ya kupata nyufa na 9,471 zimepata uharibifu mdogo huku wananchi 126,315 wakihitaji misaada mbalimbali
IMETOLEWA NA:
OFISI YA WAZIRI MKUU,
2 MTAA WA MAGOGONI,
S. L. P. 3021,
11410 DAR ES SALAAM.
JUMANNE, OKTOBA 11, 2016
No comments:
Post a Comment