Na Talib Ussi, Zanzibar
MAMLAKA ya Kuzuia Rushwa na Uhujumu Uchumi Zanzibar (ZAECA) imemkamata mwekezaji wa hoteli ya THE AIYANA’ Naraindra Sungkur raia wa Mouritius, kwa makosa ya kutolipa kodi ya ardhi mwaka 2014/2015 na mwaka 2015/2016 na deni analodaiwa ni $D 40,200 kwa makisio, ambapo ni sawa na shilingi 88,440,000 milioni za kitanzania.
Mdhamini wa Mamlaka hiyo Pemba, Suleiman Ame Jumaamesema kuwa,taasisi yake imejipanga kikamilifu kupambana na wale wote wanaojishughulisha na rushwa na uhujumu uchumi huku ikisema kuwa, hakuna atakaekwepa mkondo wa sheria iwapo atakwenda kinyume na sheria zilizowekwa na nchi.
Hayo aliyaelezwa wakati alipokua akizungumza na mwandishi wa habari hizi, kufuatia tukio la kumkamata mwekezaji huyo anayeendesha shuhuli zake Makangale Wilaya ya Micheweni Mkoa wa Kaskazini Pemba.
Mdhamini huyo alisema kuwa, kumekuwa na baadhi ya wafanyabiashara wasio waaminifu wanakwepa kulipa kodi nchini na hatimae kuikosesha serikali mapato yake na kusema kuwa, Mamlaka hiyo imejipanga vya kutosha kukabiliana na wafanyabiashara wa aina hiyo.
Suleiman alifahamisha kuwa, mara baada ya kupata taarifa hiyo, Mamlaka iliamua kumuandikia hati ya wito na iliandika hati hizo zisizopungua tatu lakini hakutii amri hiyo, ambapo kufanya hivyo ni kosa kisheria kwa mujibu wa sheria ya Kuzuia Rushwa na Uhujumu Uchumi Zanzibar.
“Kwa kipindi tofauti tumemwandikia hati hizo, lakini hakuna hata moja aliyotoa mashirikiano, yakwanza ilikuwa 12/04/2016 hakuitika, pia 27/05/2016 hakuitika na 22/06/2016 pia alipinga wito huo, hivyo leo (jana) tumeamua rasmi kwenda kumkamata ”, alisema Suleiman.
Aidha Mdhamini huyo alisema kuwa, mara baada ya kumkamata waliwasiliana na ofisi ya mkurugenzi wa mashitaka na kuwasilisha Jalada la mtuhumiwa huyo pasi na kumchelewesha, baada ya taratibu hizo kukamilika na kumpeleka mahakamani na kosa lake limesomwa na mahakama ya mkoa, hivyo mahakama hiyo haikuweza kumpatia dhamana kwa sababu sheria haina uwezo wa kusikiliza shauri hilo.
Alieleza kuwa, mtuhumiwa huyo amewekwa rumande mpaka pale kesi yake itakaposomwa tena Disemba 5 mwaka huu.
No comments:
Post a Comment