November 22, 2016

Vijana someni elimu ya Uraia

Na Talib Ussi, Zanzibar

VIJANA kisiwani Pemba wametakiwa kuisoma na kuielewa vyema elimu ya uraia, ili kuweza kufichua kero zinazowakabili na kuziwasilisha kwa viongozi wao wa majimbo, kwa lengo la kupatiwa ufumbuzi.

Akizungumza katika mkutano wa kutoa elimu hiyo kwa vijana uliofanyika katika ukumbi wa Mfuko Hifadhi ya Jamii Pemba (ZSSF), Mbunge wa viti maalum Chadema Pemba Zainab Mussa Bakar alisema, ni vyema kwa vijana kujua elimu ya uraia ili waweze kujua haki zao za msingi.

“Elimu ya uraia ni haki ya kila mwananchi, hivyo ni vyema vijana mkaisoma na kuifanyia kazi, ili muweza kuzitoa kero zinazowakabili wananchi kwa ajili ya kupatiwa ufumbuzi zaidi” alieleza Bi Zainab.

Alieleza kuwa  Kwenye majimbo kuna kero mbali mbali zinazohitaji ufumbuzi na sio rahisi kiongozi kuiziibua hivyo iwapo vijana wataisoma elimu ya uraia na kuifanyia kazi wataweza kuziibua na kuwakabidhi voningozi wao.

Alieleza kuwa, vijana wote wa Tanzania wanahitaji kupewa elimu hiyo, ili kuweza kupata taifa bora, viongozi bora na imara na raia wenye kujielewa.

Aidha aliwataka vijana hao kuisoma elimu ya sheria, kwani wataweza kujua sasa ni wakati muafaka kwa kiongozi asiefuata sheria kumwambia na kufanya mabadiliko.

Kwa upande wake Mwenyekiti wa Jukwaa la katiba Tanzania, Deus Kibamba aliwataka vijana hao kuifanyia kazi elimu hiyo, kwani wataweza kujenga hoja ya msingi ya kutetea haki zao endapo zitavunjwa.

''Mutumie hekima katika kudai haki zenu kwa viongozi, musuwatusi, kwani hiyo haitoweza kuwasaidia'', alisema Mwenyekiti huyo.

Mwenyekiti huyo alisema kuwa, lengo la mafunzo hayo ni kuwawezesha vijana kujua haki zao za msingi katika nchi.

Nae Afisa Utafiti wa Ujenzi na Demokrasia Tony Altred Kirita alieleza kuwa, wanatoa elimu ya uraia kwa wananchi wa Tanzania, ili waweze kufanya mabadiliko na kuweza kufikia maengo.

Mratibu wa Chadema Pemba, Khamis Issa Mohamed aliwataka vijana hao kuifanyia kazi elimu waliyopewa kwa kuzifichua changamoto zinazowakabili wananchi na kuona zinapatiwa ufmbuzi.

Nae mshiriki Omar Hamad Nassor mkaazi wa Chake Chake, alisema kuwa wamejifunza vitu vingi na kupata vitu vipya katika mafunzo hayo, ingawa kuifanyia kazi ni vigumu kutokana na ukandamizwaji uliopo.

Riziki Ali Mgeni mkaazi wa Mtambwe Wilaya ya Wete, aliwataka washiriki wa mkutano huo kushirikiana pamoja na kuifikisha elimu hiyo kwa wananchi, ili waweze kujielewa.

No comments:

Post a Comment

Pages