January 29, 2017

Balozi Sefue Ateuliwa Jopo la Watu Mashuhuri Afrika

Mwanadiplomasia mahiri wa Tanzania aliyepata pia kuwa Katibu Kiongozi-Ikulu, Balozi Ombeni Sefue ameteuliwa kuwa Mtanzania wa kwanza kuingia katika Jopo la Watu Mashuhuri katika Mpango wa Afrika Kujitathmini Kiutawala Bora (APRM).

Kwa mujibu wa Katibu Mtendaji wa APRM tawi la Tanzania, Rehema Twalib anayehudhuria mikutano ya Umoja wa Afrika na APRM mjini Addis Ababa, Ethiopia, Balozi Sefue ameidhinishwa kwenye kikao cha juu ya Wakuu wa Nchi za Umoja wa Afrika ambao ni wanachama wa APRM kilichofanyika juzi Jumamosi mchana.

“Haikuwa kazi rahisi kupata nafasi hii. Nchi nyingi za Afrika zilileta majina ya watu wao mashuhuri ili kuingia katika jopo hili muhimu. Balozi Sefue licha ya kuwa na utumishi uliotukuka kama mwanadiplomasia mkongwe pia aliungwa mkono kwa nguvu zote na Serikali ya Awamu ya Tano ya Tanzania,” alisema Katibu Mtendaji huyo.

APRM ni Mpango wa Afrika uliobuniwa na Wakuu wa Umoja wa Afrika kwa lengo la kuwa na chombo kitakachosaidia kuhimiza nchi wanachama kuenzi utawala bora na utoaji wa huduma bora za kiuchumi, biashara na za kujamii kwa wananchi wao kupitia mfumo wa kujitathmini zenyewe na kukosoana.

Kwa mujibu wa tovuti ya APRM, Jopo la Watu Mashuhuri ni chombo cha juu cha kuwashauri Wakuu wa Nchi Wanachama wa APRM katika uendeshaji wa Mpango huo na husimamia mchakato mzima wa kujitathmini.

Wajumbe wa jopo hilo ambao hudumu hadi miaka minne hupendekezwa na nchi zao na baada ya mchakato mrefu wenye ushindani majina ya waliokidhi vigezo huwasilishwa na kuidhinishwa na na kikao cha juu katika APRM-Mkutano wa Wakuu wa Nchi na Serikali.

Tanzania ni miongoni mwa wanachama 35 kati ya nchi 54 wa Nchi za AU zilizojiunga na APRM na ilijiunga rasmi na Mpango huo tangu mwaka 2004.Tayari Tanzania ilishafanyiwa tathmini ya kwanza ya utawala bora na inaendelea kutekeleza mapendekezo yaliyotolewa.

Katika mkutano huo Mwenyekiti wa Wakuu wa Nchi za APRM Rais Uhuru Kenyatta wa Kenya aliwapongeza wajumbe wa jopo hilo na kuwata kushiriki vyema katika kuihuisha APRM na kuwa chombo chenye thamani kubwa kwa Afrika kama walivyotarajia waasisi wake akina Thabo Mbeki, Olusegun Obasanjo, Benjamin Mkapa na wengine.

Balozi Sefue ataungana na wajumbe wengine wapya ambao ni pamoja na Prof. Ibrahim Agboola Gambari (Nigeria), Balozi Mona Omar Attia (Misri) Bi. Fatma Zohra Karadia (Algeria), Askofu Don Dinis Salomão Sengulane (Msumbiji) na Prof. Augustin Loada (Burkina Faso). Wajumbe wa zamani wanaoendelea ni pamoja na  Prof. Youssouf Khayal (Chad) ambaye kwa sasa atakuwa Mwenyekiti wa Jopo hilo na Brigitte Mabandla (Afrika Kusini) ambaye atakuwa Makamu Mwenyekiti.

Mkutano huo pia ulijadili Ripoti za tathmini za nchi katika maeneo anuai ya utawala bora kwa nchi za Kenya (ikiwa ni ripoti ya pili kuwasilishwa), Sudan, Chad, Senegal, Djibouti pamoja na ripoti ya utekelezaji ya Zambia.

No comments:

Post a Comment

Pages