January 21, 2017

BODI YA FILAMU TANZANIA YAWAKUTANISHA WADAU WAKE KWENYE KIKAO KAZI CHA KUANDAA SERA YA TAIFA YA FILAMU NCHINI


Katibu Mtendaji wa Bodi ya Filamu Tanzania Joyce Fissoo akitoa mchango wake mbele ya wajumbe wanaoshiriki kikao kazi cha maandalizi ya rasimu ya sera ya filamu nchini. Katikati ni rais wa Shirikisho la Filamu Tanzania Simon Mwakifamba.  
Wasanii na wadau wa tasnia ya filamu wanaoshiriki kikao kazi cha kuandaa rasimu ya sera ya filamu wakifurahia jambo na mwandishi mkongwe wa riwaya na miswada ya filamu Amri Bawji (mwenye baraghashia). Kikao kazi hicho kinafanyika ukumbi wa mikutano wa Taasisi ya Sanaa Bagamoyo (TaSUBA).

 Kilio cha muda mrefu cha wadau wa sekta ya filamu nchini sasa kinaelekea kupata ufumbuzi wa kudumu baada ya Bodi ya Filamu Tanzania kuwakutanisha wadau wake kwa ajili ya maandalizi ya sera mahususi itakayotoa mwongozo na kuendeleza sekta hiyo nchini.
Sekta ya filamu nchini imekuwa ikisimamiwa  na Sera ya Utamaduni na Sheria ya Filamu na Michezo ya kuigiza Na. 4  ya mwaka 1976 pamoja na kanuni zake. Kukosekana kwa sera mahususi ya filamu nchini kuliibua changamoto mbalimbali. 
Changamoto hizo ni pamoja na kuwepo kwa filamu na michezo mingi ya kuigiza inayotayarishwa chini ya viwango, kutokuwepo kwa mitaji na uwekezaji wa kutosha, sekta ya filamu kutoendeshwa kibiashara, kukosekana kwa mifumo bora ya usambazaji, kutokuwepo kwa weledi na ubunifu wa kutosha, uharamia wa kazi za filamu n.k.
Changamoto zilizoainishwa hapo juu zilibainika baada ya Bodi ya Filamu Tanzania kwa kushirikiana na wadau mbalimbali kufanya tafiti kuhusu hali halisi ya tasnia (situational analysis) na kuuwasilisha mbele ya kikao kazi cha wadau kilichofanyika tarehe 3 Oktoba, 2016 ukumbi wa uwanja wa Taifa.  Kwenye kikao hicho, Waziri wa Habari, Utamaduni, Sanaa na Michezo Mheshimiwa Nape Nnauye, aliagiza uongozi wa Bodi ya Filamu Tanzania na wizara yake kushirikiana pamoja kuhakikisha sera mahususi ya filamu inapataikana mapema iwezekanavyo.
Sera hiyo mahsusi ya filamu nchini inategemewa kuwa mwarobaini wa changamoto zinzoikabili sekta hiyo kwa muda mrefu sasa. Ikumbukwe wadau wa tasnia ya filamu nchini wamekuwa wakilalamika kukosa mapato stahili yanayotokana na kazi zao, kushindwa kupata mitaji ya kuwawezesha kuwekeza miundo mbinu ya kisasa kwenye uzalishaji na mfumo hafifu wa kupambana na uharamia wa kazi zao.

Picha na Habari
Ofisi ya Mawasiliano na Uhusiano
BODI YA FILAMU TANZANIA

No comments:

Post a Comment

Pages