January 21, 2017

UCHAGUZI WA CHAMA CHA MPIRA WA MIGUU MKOA WA RUKWA

Kamati ya Uchaguzi ya Shirikisho la Mpira wa Miguu Tanzania (TFF) iliyokutana tarehe 18/01/2017 katika ofisi za TFF pamoja na mambo mengine pia ilijadili suala la uchaguzi wa Chama cha Mpira wa Miguu Mkoa wa Rukwa (RUREFA).

Kamati ya Uchaguzi ya TFF ilizuia mchakato huo usiendelee kwa barua ya tarehe 19/12/2016 yenye kumbukumbu Na TFF/ADM/LM.184/2016, kwa sababu ya rufaa iliyowasilishwa katika kamati ya Rufaa ya Uchaguzi ya TFF.
Lakini Kamati yako ya Uchaguzi ya RUREFA ilikaidi na kuendelea na mchakato huo na hatimaye uchaguzi ulifanyika tarehe 15/01/2017 na tayari umekwisha wasilisha TFF matokeo ya uchaguzi huo.
Aidha kufanya uchaguzi wakati kuna zuio la kusitisha uchaguzi kutoka Kamati ya Uchaguzi ya TFF ni kosa la kinidhamu kwa mujibu wa kanuni za uchaguzi za wanachama wa TFF.
Hivyo basi kamati ya uchaguzi ya TFF imeamua Kama ifuatavyo:-
1.   Kuivunja kamati ya uchaguzi ya mkoa wa Rukwa Kwa mujibu wa Kanuni ya Uchaguzi ya wanachama wa TFF ibara ya 26(2).
2.   Uchaguzi uliofanyika tarehe 15/01/2017 pamoja na matokeo yake ni batili na hivyo hayatambuliwi.
3.   Kamati inaagiza kwamba katibu Mkuu wa TFF awafungilie mashitaka kwenye Kamati ya Nidhamu ya TFF viongozi wa RUREFA ambao ni Mwenyekiti wa chama cha Mpira wa Miguu Mkoa wa Rukwa, Kaimu Katibu Mkuu wa RUREFA pamoja na Mwenyekiti wa kamati ya uchaguzi ya RUREFA katika Kamati ya Nidhamu, kwa mujibu wa ibara ya 26(8) ya kanuni za uchaguzi za wanachama wa TFF.
Viongozi hao wanashitakiwa kwa kuwa walikuwa na mamlaka ya kutii maagizo kutoka vyombo vya juu, lakini kwa sababu wanazozijua wao, walikaidi.
Uchaguzi wa RUREFA utaendelea mara baada ya kupokea maelekezo kutoka Kamati ya Uchaguzi ya TFF ambayo sasa itasimamia uchaguzi wa RUREFA.
..…………………………………………………………………………........................
IMETOLEWA NA SHIRIKISHO LA MPIRA WA MIGUU TANZANIA (TFF)

No comments:

Post a Comment

Pages